[ad_1]
Kibaki kuzikwa Jumamosi, Aprili 30, 2022
NA CHARLES WASONGA
RAIS wa tatu wa Kenya marehemu Mwai Kibaki atazikwa nyumbani kwake eneo bunge la Othaya, kaunti ya Nyeri, mnamo Jumamosi Aprili 30, 2022.
Tangazo hilo limetolewa Jumamosi, Aprili 23, 2022 na Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i kwenye kikao na wanahabari nje ya jumba la Harambee jijini Nairobi.
“Mnamo Ijumaa kutakuwa na Ibada ya Kitaifa ya Wafu ya kumuaga Rais Mwai Kibaki katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, Nairobi,” Dkt Matiang’i akasema.
Kabla ya hapo mwili wa marehemu utalazwa katika Bunge la Kitaifa ambako wananchi watapa nafasi ya kutoa heshima zao kwa siku tatu kuanzia Jumatatu hadi Jumatano.
“Vile vile, vitabu vya rambirambi pia vitawekwa katika Bunge la Kitaifa, Bunge la Seneti, makao makuu ya maeneo manane ya kanda na kaunti zote 47,” Dkt Matiang’i akasema.
Waziri huyo pia aliongeza kuwa kitabu kingine cha rambirambi kitawekwa katika Afisi ya CDF mjini Othaya ambako wakazi wa Nyeri na eneo zima la Mlima Kenya watafika kutoa pole zao.
“Vitabu vingine pia vitawekwa katika Afisi ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni kwa mabalozi wa mataifa ya kigeni kutoa rambirambi zao,” akasema Dkt Matiang’i.
“Raia wa hadhi ya juu pia watapata nafasi ya kutoa pole zao kwa familia ya Kibaki katika afisi zake za Nyeri. Maelezo kuhusu namna Wakenya watakavyofikia afisi hizo yatatolewa. Hiyo itafanyika siku mbili kuanzia Jumanne hadi Jumatano,” akaongeza.
Mzee Kibaki alifariki mnamo Ijumaa, Aprili 22, 2022 akiwa na umri wa miaka 90.
Next article
TAHARIRI: Heko za dhati wanamichezo kwa kuchochea chipukizi…
[ad_2]
Source link