Kikao cha Kibaki chageuzwa uwanja wa Azimio na Kenya Kwanza kututumua misuli
NA CHARLES WASONGA
WABUNGE wa mirengo ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza walionyesha mfano mbaya kwa kugeuza kikao maalum cha kumwomboleza Hayati Mwai Kibaki kama uwanja wa kuvumisha wagombeaji urais wa miungano yao.
Wabunge wa Kenya Kwanza wanaounga mkono azma ya urais ya Naibu Rais William Ruto walimshutumu Rais Uhuru Kenyatta kwa kumuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.
Wakiongozwa na Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale, wabunge hao, Rigathi Gachagua (Mathira), Ndindi Nyoro (Kiharu) na Kimani Ichung’wa (Kikuyu) walimtaka Rais Kenyatta kuiga mfano wa Kibaki kwa kutojihusisha na siasa za urithi wake.
“Kibaki alikuwa kiongozi shupavu ambaye aliweka mbele mipango ya ufufuaji uchumi. Na wakati wake wa kuondoka afisini ulipotimu, hatukumuona akiingilia sasa za urithi wake inavyofanyika sasa,” akasema Bw Duale.
“Kwa hivyo, kwa heshima ya Rais Kibaki, tunamwomba Rais wa sasa ajiondoe kabisa katika siasa za kinyang’anyiro cha urais. Ajiandae kustaafu kwa upole na taadhima,” akaongeza.
Naye Bw Ichung’wa alishutumu Rais Kenyatta kwa kuiwekea nchini hii mzigo mzito wa madeni kwa kupokoa bila mpango maalum.
“Rais Kibaki amekufa akiwa mwenye huzuni kuu. Hii ni kwa sababu mrithi wake ameporomosha uchumi ambao aliuacha ukiwa thabiti kwa kukopa zaidi kutoka mataifa ya kigeni. Kibaki alipoondoka afisini, Kenya ilikuwa na mzigo wa madeni wa kima cha Sh1.6 trilioni pekee. Lakini inasikitisha kuwa chini ya utawala wa handisheki, kiwango cha madeni kimefikia trilioni 8.6,” Mbunge huyo wa Kikuyu akasema.
Bw Ichung’wa ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti alisema kuwa kando na deni hilo la Sh8.6 trilioni, mashariki ya serikali yamekopa Sh3 bilioni kutoka nje, kupitia udhamini wa serikali.
“Kibaki hakuamini kuwa njia ya kupekee ya kufadhili miradi ya serikali ni kupitia mikopo bali pesa ambazo huzalishwa ndani ya nchi. Sasa Kenya imesakamwa na mikopo hali ambayo imechangia kupanda kwa gharama ya maisha,” akasema Bw Nyoro, ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kiuchumi.
Lakini wabunge wa mrengo wa Azimio walijibu kwa kusema kuwa Dkt Ruto anajulikana kwa kutomheshimu Rais, kinyume na Kibaki ambaye hakuwa na shida yoyote ya bosi wake, Daniel Moi, hata alipopokonywa wadhifa wa makamu wa rais.
Wabunge hao Emmanuel Wangwe (Navakholo), Moitalel Ole Kenta (Narok Kaskazini) na Opiyo Wandayi (Ugnjwa) ,wa Azimio ,walisema Kibaki alikuwa na bahati nzuri kwa kuwa na makamu watiifu.
“Kibaki alikuwa na bahati kwa sababu alihudumu na makamu watiifu. Sio kama leo ambapo Naibu Rais amegeuka kuwa kiongozi wa upinzani katika serikali ambayo anaihudumia,” Bw Wandayi akasema.
Bw Wangwe alisema Hayati Kibaki hakukabiliwa na changamoto zozote alipohudumu kama rais. Rais Kibaki alikuwa na makami watatu, marehemu Wamalwa Kijana, Moody Awori na Kalonzo Musyoka.
“Makamu hawa wote walikuwa watiifu kwa Kibaki sio Ruto ambaye humzomea mkubwa wake hadharani. Naibu Rais yuko ya pupa ya kuwa Rais wa Kenya jambo ambalo halikushuhudiwa wakati wa utawala wa Rais Kibaki,” akaongeza Bw Wangwe ambaye ni kiranja wa wengi.
Hata hivyo, wabunge wa pande zote mbili walikubaliana kwamba Hayati Kibaki alikuwa mchapakazi ambaye aliwezesha uchumi kuimarika na kuwezesha Kenya kupata Katiba Mpya mnamo Agosti, 2010.