Kinyang’anyiro cha ugavana Kakamega kuzua kivumbi kikali
NA BENSON AMADALA
KITI cha ugavana katika Kaunti ya Kakamega kimezua ushindani mkubwa miongoni mwa wawaniaji wa vyama vya ODM, ANC na DAP-K.
Bendera ya ODM inapeperushwa na aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa kampuni ya kusambaza umeme, Ketraco, Fernandes Barasa huku seneta wa sasa wa kaunti hiyo, Cleophas Malala akijaribu kutwaa kiti hicho kwa tiketi ya ANC.
Kwa upande wake Naibu Gavana Philip Kutima ambaye aligura ODM mwezi Machi anawania kiti hicho kwa tiketi ya DAP-K.
Profesa Kutima aligura chama hicho cha Chungwa baada ya kudai kuwa bosi wake, Gavana Wycliffe Oparanya, alikuwa akihujumu ndoto yake ya kuwa mrithi wake.
Mwezi huo wa Machi, kiongozi wa ODM Raila Odinga alimwidhinisha Bw Barasa kama chaguo la chama kwa wadhifa huo alipozuru kaunti ya Kakamega kwa ziara ya kusaka uungwaji mkono.
Lakini uamuzi huo umeibua malalamishi kutoka kwa wanasiasa wengi katika kambi ya Bw Odinga ambao walikuwa wakimezea mate kiti hicho.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Shinyalu, Bw Justus Kizito.
Mbunge huyo ambaye alichukua hatamu za uenyekiti wa ODM kaunti ya Kakamega baada ya Prof Kutima kuhamia chama cha DAP-K, alikuwa ametangaza kuwa angeshiriki kura ya mchujo ya ODM kusaka tikiti ya kuwania wadhifa wa ugavana.
Gavana Oparanya, ambaye ni naibu kiongozi wa ODM, pia analaumiwa kwa kupanga hatua ya chama hicho kutoa vyeti vya moja kwa moja kwa wabunge kadha waliojiunga na ODM baada ya kugura vyama vya ANC na DAP-K.
Wale waliopokezwa vyeti vya uteuzi wakati wa ziara hiyo ya Bw Odinga ni wabunge; Tindi Mwale (Butere), Christopher Aseka (Khwisero), Titus Khamala (Lurambi), Peter Nabulindo (Matungu) na Emmanuel Wangwe (Navakholo).
Inasemekana kuwa ODM ilitegemea kura ya maoni iliyoonyesha kuwa wabunge hao walikuwa maarufu miongoni mwa wawaniaji wa viti hivi katika maeneo husika.
Wawaniaji wengine wa ODM katika maeneo bunge ya Malava, Mumias Magharibi, Lugari na Likuyani watapambana katika kura ya mchujo itakayofanyika Alhamisi juma lijalo.
Mbunge wa Lugari, Bw Ayub Savula, mnamo Jumanne alishikilia kuwa yuko katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kakamega kwa tiketi ya DAP-K. Hii ni licha ya kwamba awali, ilisemekana kuwa tikiti hiyo ingemwendea Prof Kutima.