Connect with us

General News

Kiti moto cha useneta Mombasa chavutia 14 – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Kiti moto cha useneta Mombasa chavutia 14 – Taifa Leo

Kiti moto cha useneta Mombasa chavutia 14

NA WACHIRA MWANGI

KINYANG’ANYIRO cha kiti cha useneta Kaunti ya Mombasa kimewavutia wawaniaji 14.

Huku ikibakia miezi miwili uchaguzi Mkuu ufanyike, kiti hicho kina wawaniaji huru watatu pekee wanaolenga kumrithi seneta wa Kaunti hiyo, Mohamed Faki.

Shughuli ya kuwaithinisha watakaowania kiti hicho na Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), ilianza Jumapili.

Tayari wawaniaji watano Elisha Kilale (chama cha Tujibebe), Hisham Mwidau (mwaniaji huru), Miraj Abdalla (PAA), Hazel Katana (Jubilee) na Margaret Masiko (DAP-K) tayari wameshaidhinishwa na IEBC.

Jumatatu, IEBC ilitarajiwa kuwaidhinisha wawaniaji wengine watano ambao ni Abdulsalam Kassim (Wiper), Charles Bwire (ANC), Al-Amin Somo (mgombea huru), Hamisi Mwaguya (UDA) na Joyce Mwangoma (Safina).

Jumatano, seneta wa kaunti hiyo, Mohamed Faki (ODM), Mohamed Amir (mgombea huru), Peterson Mitau (Maendeleo Chap Chap), na Cornelius walifaa kufika mbele ya tume ya IEBC kwa shughuli iyo hiyo.

Kinyang’anyiro hicho kitakuwa cha kufa na kupona kati ya wagombea watatu, Faki, Mwaguya na Kassim wote wanaotoka katika vyama maarufu.Hamisi Mwaguya ambaye ni mwaniaji kupitia tikiti ya UDA alisema kuwa chama chao kinalenga kuwakomboa wakazi wa kaunti hiyo kwa utawala mbaya wa chama cha ODM.

“Tunashukuru Mungu kuwa tayari tumeidhinishwa kuwania kiti hicho. Chama cha UDA ndicho kitakachowakomboa wakazi wa Mombasa dhidi ya utawala mbaya wa ODM. Serikali yangu itawatetea wakazi wa Mombasa na kuhakikisha kuwa uchumi wa kaunti unaimarika,” akasema Bw Mwaguya.

Mwaniaji huyo alidai kuwa chama chao cha UDA kinanuia kuwaunganisha wakazi wa Mombasa.Kwa upande wake, mwaniaji huru, Mohamed Amir, alisema ana uhakika wakazi wa kaunti hiyo watamchagua.

“Tuko tayari hasa baada ya kuidhinishwa na IEBC. Wakazi wa Mombasa watakuwa na seneta mwenye bidii baada ya Agosti 9,” akasema Bw Amir.

Kadhalika, aliwarai wakazi kutompigia mtu kura kwa sababu ya chama chake bali waangazie utendakazi wa mtu binafsi.

“Kura yako ndio kesho yako. Msimchague mtu kwa sababu ya pesa au chama. Hakikisha utakayechaguliwa ana uwezo wa kuleta maendeleo na kuboresha maisha,” akasema Bw Amir.

Naye seneta wa Mombasa Mohamed Faki ambaye anatetea kiti chake aliahidi kuwatumikia wakazi wa kaunti hiyo na hata kuboresha maisha yao zaidi.