Kiwango cha uzalishaji nyama ya ng’ombe kimeshuka nchini ila hakuna uhaba – Katibu Kimtai
NA SAMMY WAWERU
KIWANGO cha uzalishaji wa nyama ya ng’ombe kimeshuka kwa kiasi kikubwa kufuatia ukame unaoshuhudiwa katika kaunti 24 nchini.
Maeneo kame (ASAL), yanayoendeleza ufugaji yanategemewa pakubwa katika uzalishaji wa nyama ila baa la njaa limesababisha mifugo kufariki na katika baadhi ya kaunti kusombwa na maji kufuatia mafuriko yanayoshuhudiwa.
Katibu katika Wizara ya Mifugo, Bw Harry Kimtai amefichua kiwango cha nyama kimeshuka kwa tani 340, 000 (kipimo cha Metric tons).
“Chini ya Ajenda Nne Kuu, lengo letu kama taifa limekuwa kuongeza uzalishaji wa nyama kutoka tani 720, 000 (kiwango cha sasa) hadi tani 990, 000.
“Japo, kwa ajili ya kiangazi katika maeneo kame, kiwango cha uzalishaji kimepungua kwa tani 340, 000 kwa sababu yavmifugo kufariki,” Bw Kimtai akaambia Taifa Leo katika mahojiano ya kipekee afisini mwake Kilimo House, Jijini Nairobi.
Athari za mabadiliko ya tabianchi (climate change), zimechangia kukithiri kwa ukame.
Kulingana na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO – UN), Kenya ni miongoni mwa nchi tatu Upembe wa Afrika zilizolemewa na makali ya ukame.
Mataifa mengine ni Ethiopia na Somalia, FAO ikionya endapo hatua za dharura hazitachukuliwa kufikia Juni mwaka huu, huenda mamilioni ya watu wakakosa chakula.
“Ni muhimu kukumbusha taifa ukame umekuwa ratiba ya kila mwaka, hali ya anga imebadilika,” Kimtai akasema.
Licha ya Kenya kuandikisha kushuka kwa uzalishaji wa nyama ya ng’ombe, afisa huyo alithibitisha taifa lina nyama ya kutosha.
Alisema wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi wowote, kwa kile alitaja “upungufu ulioko hauibui hofu kwa lolote lile”.
“Ni upungufu unaoleta mianya ya ufanisi, hususan kwa wafugaji wa kuku, mbuzi, samaki, kondoo na nguruwe,” Katibu akaelezea.
“Nyama tunazozalisha zinakithi mahitaji yaliyoko.”
Huku athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwa bayana, hasa baada ya msimu wa mvua kubwa kukawia na kuanza juma lililopita badala ya mwezi wa Machi, Kimtai alisema serikali imeweka mikakati maalum kuangazia changamoto zinazokumba maeneo kame.
Alisema, imeanza kutathmini mikakati iliyokuwa ikitumika awali na kujumuisha sekta ya kibinafsi.
“Tunahamasisha kampuni na mashirika ya kibinafsi kushirikiana na sekta ya umma na wadauhusika, kukusanya fedha kuboresha kilimo na ufugaji,” akafafanua.
“Wadau katika sekta ya kibinafsi wataleta mchango mkubwa kuokoa jamii zinazoendeleza ufugaji, na kusaidia kuimarisha uzalishaji nyama nchini,” akasema.
Alisema mpango huo unajumuisha uanzishaji maeneo ya kulishia mifugo, kupitia upanzi wa nyasi na majani.
Alifichua, tayari Kaunti ya Kwale, Kajiado na Garissa, wawekezaji wa kibinafsi wamekumbatia mfumo huo kuokoa mifugo.
Isitoshe, Katibu alidokeza kwamba baadhi ya wafugaji wameanza kupanda malisho Kaunti ya Kajiado, akihimiza waige mkondo huo akisistiza “haijalishi iwapo ni ranchi kubwa au ndogo”.
Ranchi, ni eneo maalum lililotengewa upanzi wa nyasi au malisho ya mifugo.
Huku wafugaji maeneo kame wakikadiria hasara ya mifugo wao kufa njaa, Bw Kimtai alisema idara ya mifugo kupitia Shirika la Nyama Nchini (KMC), inajaribu iwezavyo kuikoa – Kuchinja ng’ombe walionusurika.
Vilevile, alisema imezindua Mpango wa Fidia – Kenya Livestock Insurance Program (KLIP).