[ad_1]
Kocha Louis Van Gaal afichua anaugua saratani ya kibofu
Na MASHIRIKA
MKUFUNZI wa zamani wa Manchester United ambaye sasa anadhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Uholanzi, Louis van Gaal, amefichua kwamba ana saratani ya kibofu.
Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 70 alielezea hali yake ya kuugua katika mahojiano ya kipindi cha Humberto kilichoandaliwa na runinga moja nchini Uholanzi mnamo Aprili 3, 2022.
“Sikutaka kuwaambia wachezaji wangu kwa sababu hatua hiyo ingeathiri matokeo yao katika mechi kadhaa zilizopita,” akasema Van Gaal.
Hii ni awamu ya tatu ambapo Van Gaal anadhibiti mikoba ya Uholanzi. Aliwaongoza kukamilisha kampeni za Kombe la Dunia za 2014 nchini Ujerumani hadi nafasi ya tatu. Sasa anatarajiwa pia kusimamia kikosi hicho cha Uholanzi wakati wa fainali za Kombe la Dunia mnamo Novemba na Disemba 2022 nchini Qatar. Kikosi chake kimetiwa katika Kundi A pamoja na Senegal, Ecuador na wenyeji Qatar.
“Katika mara zote ambapo nimekuwa kocha wa timu ya taifa, ningeondoka kambini kwenda hospitalini usiku bila wachezaji wangu kufahamu lolote,” akasema Van Gaal.
Katika kipindi cha misimu miwili ya kuhudumu kwake ugani Old Trafford, Van Gaal aliongoza miamba hao kutwaa Kombe la FA mnamo 2016 kabla ya nafasi yake kutwaliwa na kocha Jose Mourinho.
Amewahi pia kuzoa mataji ya Ligi Kuu akidhibiti mikoba ya Barcelona, Bayern Munich, AZ Alkmaar na Ajax aliowangoza kunyanyua ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 1995.
Van Gaal alizolea Ajax taji hilo la UEFA mwaka mmoja baada ya mkewe wa kwanza, Fernanda Obbes kuaga dunia kutokana na saratani ya maini na kongosho.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
[ad_2]
Source link