KRU yatarajiwa Ijumaa kutangaza adhabu dhidi ya wachezaji, kocha wa Shamas
Na GEOFFREY ANENE
SHIRIKISHO la Raga Kenya (KRU) linatarajiwa Ijumaa kutangaza adhabu yake kwa wachezaji watatu na kocha kutoka klabu ya Shamas walioshambulia refa Said Kenya katika nusu-fainali dhidi ya Catholic Monks mnamo Machi 19.
Shirikisho hilo limesema limekamilisha uchunguzi wake dhidi ya wanne hao waliofanya kitendo hicho baada ya Shamas kupoteza tiketi ya kupandishwa kushiriki Ligi Kuu (Kenya Cup) ya msimu ujao kwa kulemewa 9-5 na Monks uwanjani RFUEA.
Hatua itakayochukuliwa na KRU itakuja siku chache baada ya Shamas kufuta kazi kocha Stephan Outtou na washambulizi watatu.
Sababu ya Shamas kukatiza uhusiano na Outtou, ambaye anatoka Magharibi mwa Afrika, na wachezaji Wakenya James Kang’ethe na Joseph Kang’ethe, ambao ni ndugu, na Julian Ouma, ni tukio wakati wa nusu-fainali dhidi ya Monks jijini Nairobi ambapo Kenya alishambuliwa.
Kang’ethe wote wawili, ambao ni pacha, waliwahi kuchezea timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande maarufu kama Kenya Simbas miaka chache iliyopita.
Monks ilishinda Shamas 9-5 na kujikatia tiketi ya kushiriki Kenya Cup msimu ujao wa 2022-2023.
Shamas ilichukua hatua hiyo huku paneli ya uamuzi ya KRU inayojumuisha maafisa George Mbaye, Aggrey Chebeda na Duncan Ndegwa, ikiendelea kusikiza kesi hiyo kabla ya shirikisho kusema uamuzi utatangazwa Ijumaa.
Mwanzilishi wa taasisi ya raga ya Shamas, Azim Deen alisema katika taarifa Jumanne kuwa uamuzi wa kuwaondoa kazini wanne hao ukifikiwa baada ya viongozi kukutana kufuatia visa hivyo vya kusikitisha.
Deen alisema, “Watu wanne tuliotaja hapo juu hawana uhusiano na shirika letu na hawaruhusiwi kufanya shughuli yoyote kwa niaba ya Shamas.”
Aliongeza kuwa utamaduni wa Shamas hauruhusu tabia kama hiyo.
KRU na Chama cha Marefa wa Raga Kenya (KRRA) kupitia Katibu Mkuu Ian Mugambi na Rais Mwangi Karimi mtawalia, wamelaani kisa hicho ambapo Kenya alishambuliwa na wachezaji hao kipenga cha mwisho kilipolia. Kang’ethe wote wawili walikuwa wameonyeshwa kadi ya njano dakika ya 78 na kukaa nje kwa dakika mbili zilizokuwa zimesalia.
Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi ililemea South Coast Pirates katika nusu-fainali nyingine iliyochezewa Ukunda pia kuingia Kenya Cup. Monks na Machine zilijaza nafasi ya miamba Impala Saracens na Nondescripts waliokamata nafasi mbili za mwisho kwenye Ligi Kuu na kutemwa.