WANDERI KAMAU: Uchumi: Kuna uwezekano Serikali inawapotosha raia
NA WANDERI KAMAU
KUTOKANA na maendeleo ya kiteknolojia, usambazaji wa habari duniani umebadilika kabisa.
Kwa sasa, ni rahisi mtu kujua mambo tofauti yanayoendelea duniani akiwa popote alipo, bora tu awe na rununu, kompyuta au kipakatalishi kilichounganishwa na mtandao wa intaneti.
Kwa hilo pekee, itakuwa rahisi kwake kujua yale yanayofanyika barani Asia, Ulaya, Amerika (Kusini na Kaskazini), Australia na kwingineko.
Hapo awali, ilikuwa vigumu sana kufuatilia wala kufahamu yanayoendelea duniani.
Ilimlazimu mtu kuwa na redio yenye uwezo wa kunasa mawimbi ya vituo vya habari vya kimataifa kama vile BBC, Sauti ya Amerika (VoA), Deutsche Welle (DW), Redio China Kimataifa (CRI), Sauti ya Iran kati ya vingine vingi.
Ijapokuwa ujio wa mtandao wa intaneti umerahisisha sana usambazaji habari duniani, vile vile umechangia sana kudidimia kwa maadili na kusambaa kwa uhalifu na upotoshaji kwa karibu viwango vyote.
Kwa sasa, ni vigumu kutofautisha habari za kweli na uwongo ikiwa mtu hana uelewa wa kina kuhusu masuala yanayoendelea.
Mbali na mitandao, taasisi muhimu za serikali pia zimejipata pabaya kwa madai ya kutoa takwimu ama habari ambazo hazilingani na uhalisia uliopo.
Kwa mfano, Shirika la Takwimu Kenya (KNBS) limejipata matatani kwa tuhuma za kutoa takwimu “za uwongo” kuhusu ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kulingana na takwimu zilizotolewa na shirika hilo wiki iliyopita, uchumi wa Kenya ulikua kwa asilimia saba mwaka 2021.
Hata hivyo, Wakenya wengi wanashikilia kuwa huenda takwimu hizo zisiwe za kweli, kwani hali ya maisha inaendelea kuzorota nchini.
Wengi wanasema kuwa tangu mwaka wa 2020, gharama ya maisha imepanda kwa kiasi ambacho hakijawahi kushuhudiwa hapo awali.
Swali ni, je, ni nani msema kweli kati ya serikali na Wakenya?
Ikiwa uchumi umekua, walionufaika nao hasa ni akina nani? Ni raia ama watu wachache tu wanaodhibiti sekta muhimu za kiuchumi
Kutokana na tashwishi ambazo zimeibuliwa, ni wakati mwafaka kwa KNBS kujitokeza wazi kueleza taratibu ilizotumia kukusanya takwimu hizo, kwani si taswira nzuri wakati raia wanapinga ama kutoamini maelezo yanayotolewa na serikali yao kuhusu mwelekeo wa nchi.
Haifai hata kidogo.
Kimsingi, kunapaswa kuwa na hali ya kuaminiana kati ya serikali na raia. Uaminifu huo ndio nguzo kuu ambayo huwa kama injini ya kuiendesha nchi.
Bila uwepo wake, ni jambo hatari sana ambalo huenda likavuruga msingi, uthabiti na mwelekeo wa nchi.
Taswira kama hizo ndizo huibua maasi ya raia dhidi ya serikali au tawala zilizopo.
Ni taswira iliyoshuhudiwa wakati wa maasi yaliyotokea katika mataifa ya Arabuni kama Tunisia, Misri na Libya kuanzia 2011, ambapo viongozi maarufu walipinduliwa mamlakani kutokana na ghadhabu za raia.
Katika hali ambapo baadhi ya taasisi zimekuwa zikilaumiwa kwa “kuipendelea” serikali, ni wakati mzuri kwa KNBS kueleza kwa kina taratibu ilizotumia kubaini uchumi wa Kenya umekua wakati raia wanateseka.
[email protected]