STEVE ITELA: KWS ibuni mbinu za kisasa kukabili mzozo wa wanadamu na wanyamapori
NA STEVE ITELA
KULINGANA na Shirika la Wanyamapori (KWS) kati ya mwaka 2017 na 2020, jumla ya Wakenya 388 waliuawa kwa kushambuliwa na wanyamapori.
Watu wengine 2,080 waliachwa wakiwa na majeraha.
Huenda miaka miwili tangu takwimu hizi zitolewe, kuna wengine wengi waliojipata katika hali sawa na hiyo. Serikali kupitia wizara ya Utalii na Uhifadhi wa Wanyamapori ilitoa jumla ya Sh530 milioni za kuwafidia waathiriwa.
Kutolewa kwa fidia hiyo ni hatua nzuri, lakini katu hakuwezi kufidia majeraha ya kudumu au mauti. Hakuna familia inayosherehekea kwa kupokea pesa baada ya kufiwa na mpendwa wao.
Ripoti iliyotolewa na Afisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Mihadarati na Uhalifu (UNODC) mwaka 2020 inaonyesha kwamba katia eneo la Kati, Mashariki na Kusini mwa Afrika pekee, ndovu 17,000 waliuawa kila mwaka kati ya mwaka 2006 na 2018.
Hii ina maana kuwa kwa jumla eneo hili lilipoteza ndovu 204,000 katika kipindi hicho cha miaka 12. Mwaka 2018 pekee, ndovu 386 waliuawa hapa Kenya.
Takwimu hizi zinaonyesha wazi kuwa kwenye mzozo wa binadamu na Wanyama, pande zote mbili huathirika.
Ongezeko la idadi ya watu pamoja na wanadamu kuendeleza shughuli zao maeneo ya msitu, vimechangia kufungwa kwa njia za Wanyama kupita. Hali hii inapunguza eneo la Wanyama kuishi.
Kukosekana kwa makao ya Wanyama bila shaka kunazua mtafaruku huu. Jambo hili lilalazimu wadau kujikuna vichwa na kuja na mbinu za kisasa za kuutatua.
Baadhi ya mbinu ambazo KWS inaweza kuzibuni ni pamoja na kuwazuia wanyama kutangamana na wanadamu, bila ya kutumia nguvu. Hapo ndipo nchi itafanikiwa kuzuia hali ambapo wanadamu na wanyama wanawindana.
Bw Itela ni Afisa Mkuu wa Conservation Alliance of Kenya (CAK)