SERIKALI imetangaza tarehe mpya ya kufunguliwa kwa bandari ya Lamu (Lapsset) iliyoko eneo la Kililana.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua ujenzi na maendeleo ya Bandari ya Lamu Alhamisi, Waziri wa Fedha, Ukur Yatani alisema badala ya tarehe ya awali ya Juni 2021, bandari ya Lamu sasa itafunguliwa kufikia Mei 30, 2021.
Bw Yatani alisema mipango yote ya kuwezesha bandari ya Lamu kuanza shughuli zake imekamilika na kwamba wanatarajia meli ya kwanza ya mizigo kutia nanga bandarini Lamu kufikia Mei 20, 2021.
Alisema kufikia sasa kiegesho cha kwanza cha mizigo bandarini Lamu kimekamilika nacho cha pili na kile cha tatu, vitakamilika kufikia mwishoni mwa Oktoba 2021.
Waziri huyo alisema serikali imepeleka vifaa vyote vinavyohitajika kuwezesha bandari ya Lamu kuendeleza shughuli zake.
Alisema Halmashauri ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA) pia imeajiri wafanyakazi wa kutosha na kuwapa vifaa vifaavyo ili kusaidia katika uendelezaji na ufanisi wa bandari hiyo.
“Leo tumezuru eneo la mradi kutathmini ujenzi unavyoendelea na iwapo kuna uwezekano wa Bandari ya Lamu kuanza shughuli zake hivi karibuni. Nafurahi kuwatangazia kwamba serikali iko tayari na Bandari ya Lamu itafunguliwa rasmi Mei 30, 2021. Isitoshe, tunatarajia meli ya kwanza ya mizigo kutua bandarini hapa Mei 20 kuashiria mwanzo wa shughuli za bandari ya Lamu,” akasema Bw Yatani.
Mbali na kukagua ujenzi wa bandari hiyo, waziri pia alikutana na wadau wa kibinafsi, hasa wamiliki wa kampuni za uchukuzi wa bandarini, ambapo aliwahakikishia uhusiano mwema na utendakazi bora punde bandari ya Lamu itakapofunguliwa rasmi mwezi huu wa Mei.
“Tumejadiliana na wadau wa kibinafsi, ikiwemo wamiliki wa kampuni za uchukuzi wa bandarini. Tumeafikiana kwamba tusaidiane katika masuala ya miundomsingi hasa kwenye awamu ya kwanza ya utendakazi wa Bandari ya Lamu hadi pale itakapopata uwezo wa kujisimamia kushindana na bandari ya Mombasa,” akasema Bw Yatani.
Alisema katika harakati za kuhakikisha bandari ya Lamu inafikiwa kwa urahisi, serikali imekuwa ikiendeleza ujenzi wa barabara mbalimbali eneo hilo.
“Barabara ya Lamu-Witu-Garsen imebakia asilimia chache. Tunatarajia kwamba kufikia katikati ya mwezi Juni iwe yote imekamilika. Serikali pia imetoa tenda ya ujenzi wa barabara ya Lamu hadi Garissa. Haya yote yanatekelezwa ili kurahisisha uchukuzi kutoka na kuingia Lapsset,” akasema Bw Yatani.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya KPA, Joseph Kibwana, aliutaja mradi wa bandari ya Lamu kuwa wenye uwezo mkubwa wa kuajiri vijana wa ndani na nje ya eneo hilo.
Sehemu mojawapo ya mradi wa Lapsset. Picha/ Kalume Kazungu
Aliwataka wananchi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha bandari ya Lamu inaafikia malengo yake.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Lapsset, Titus Ibui, alisema kufunguliwa kwa bandari ya Lamu kutawezesha eneo hilo la kaskazini mwa Kenya kufunguka kibiashara na kiviwanda.
“Bandari ya Lamu ikianza kazi itapanua biashara kwenye eneo hili la kaskazini mwa Kenya, hivyo kuinua maisha ya wakazi wa hapa,” akasema Bw Ibui.