Liverpool kigezoni dhidi ya Aston Villa
Na MASHIRIKA
NDOTO ya Liverpool kutia kapuni taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu itazimika leo Jumanne iwapo watazidiwa maarifa na Aston Villa ya kocha Steven Gerrard uwanjani Villa Park.
Gerrard, 41, aliwahi kuchezea Liverpool (1989-2015) na LA Galaxy ya Amerika (2015-16) kabla ya kujitosa katika ulingo wa ukufunzi.
Tofauti na Liverpool ambao wana kibarua kizito cha kujinyanyua baada ya Tottenham Hotspur kuwalazimishia sare ya 1-1 ugani Anfield wikendi, Villa wana kiu ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi dhidi ya Norwich City (2-0) na Burnley (3-1) katika mechi mbili zilizopita.
Villa wamejizolea alama saba kutokana na mechi tatu zilizopita za EPL huku wakifungwa bao moja pekee.
Matokeo hayo yamewakweza hadi nafasi ya 11 jedwalini kwa alama 43 sawa na Brentford na Newcastle United waliopokezwa kichapo cha 5-0 kutoka kwa Manchester City mnamo Jumapili ugani Etihad.
Ushindi huo wa Man-City uliwarejesha kileleni mwa jedwali kwa alama 86, tatu zaidi kuliko Liverpool wanaofukuzia mataji matatu zaidi muhula huu baada ya kupepeta Chelsea kwa penalti 11-10 mwishoni mwa Februari ugani Wembley na kunyanyua Carabao Cup.
Zaidi ya kuwania taji la EPL, Liverpool watavaana na Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA mnamo Jumamosi ugani Wembley kabla ya kutoana jasho na Real Madrid ya Uhispania kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayochezewa jijini Paris, Ufaransa mnamo Mei 28.
Tofauti na Man-City ambao wametikisa nyavu za wapinzani wao mara 89 na kufungwa mabao 21, Liverpool wamepachika wavuni magoli 87 na kuokota mpira kimiani mara 23.
Jumatano itakuwa zamu ya Man-City kumenyana na Wolves kabla ya kuvaana na West Ham United na Villa.
Liverpool watafunga kampeni za EPL muhula huu dhidi ya Southampton na Wolves kwa usanjari huo.
Licha ya Villa kupigiwa upatu wa kuzamisha chombo cha Liverpool, kikosi hicho kimeshinda mechi mbili pekee kati ya nane zilizopita katika uwanja wa nyumbani.
Sare dhidi ya Spurs ilikomesha rekodi ya Liverpool ya kushinda mechi sita mfululizo katika mashindano yote na 12 mfululizo katika EPL ugani Anfield.