LIVERPOOL walipaa hadi kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupokeza Manchester United kichapo cha 4-0 mnamo Jumanne usiku ugani Anfield.
Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool sasa wanajivunia alama 76, mbili zaidi kuliko nambari mbili Manchester City ambao watarejea kileleni iwapo watatandika Brighton katika mojawapo ya mechi za EPL zitakazosakatwa Jumatano usiku.
Ushindi wa Liverpool uliweka hai matumaini yao ya kukamilisha kampeni za msimu huu wakiwa na mataji manne kabatini mwao. Mbali na kufukizia taji la EPL kwa mara ya 20 katika historia, miamba hao wanawania pia ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Kombe la FA. Tayari wamejizolea taji la Carabao Cup baada ya kupiga Chelsea kwa penalti 11-1o baada ya sare tasa kwenye fainali ya Februari 27, 2022 ugani Wembley.
Kudhalilishwa kwa Man-United ni ishara ya ukubwa wa kazi inayomsubiri kocha wao mpya, Erik ten Hag ugani Old Trafford. Mabingwa hao mara 20 wa EPL walizidiwa maarifa katika kila idara huku Liverpool wakitamalaki mechi na kumiliki asilimia kubwa ya mpira.
Man-United walikosa huduma za nyota Cristiano Ronaldo ambaye alimpoteza mwanawe wa kiume aliyezaliwa majuzi. Mashabiki wa pande zote mbili walitoa ishara ya kusimama na sogora huyo wa zamani wa Real Madrid na Juventus kwa kumpigia makofi ugani Anfield katika dakika ya saba ya mechi.
Liverpool walikuwa tayari kifua mbele wakati huo kupitia kwa bao la Luis Diaz aliyeshirikiana vilivyo na Mohamed Salah aliyefunga la pili. Bao la tatu la Liverpool lilifumwa kimiani na Sadio Mane kabla ya Salah kufunga la nne.
Walipokuwa wenyeji wa Liverpool ugani Old Trafford mnamo Oktoba 2021, Man-United walipondwa kwa mabao 5-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL msimu huu. Liverpool sasa ndicho kikosi cha kwanza kuwahi kufunga Man-United zaidi ya mabao manane
Man-United kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 54 sawa na nambari tano Arsenal watakaomenyana na Chelsea ugani Stamford Bridge mnamo Aprili 20, 2022.
Liverpool wavaana na Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA msimu huu baada ya kupimana ubabe na Villarreal ya Uhispania kwenye mikondo miwili ya nusu-fainali ya UEFA.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
[ad_2]
Source link