Connect with us

General News

Maafisa wa elimu wakae ange kuzuia visa vya udanganyifu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Maafisa wa elimu wakae ange kuzuia visa vya udanganyifu – Taifa Leo

WANTO WARUI: Maafisa wa elimu wakae ange kuzuia visa vya udanganyifu

Na WANTO WARUI

Ni wakati mwingine ambapo taifa letu linaingia katika kipindi cha mitihani hasa ule wa Darasa la Nane (KCPE) na ule wa Kidato cha Nne (KCSE), mitihani ambayo matokeo yake hungojewa kwa hamu kubwa na Wakenya wengi kutoka kila upande wa nchi.

Mtihani wa KCPE ndio utakaotangulia Machi 4 ambayo ni siku ya watahiniwa wote kukaguliwa na kuongozwa kufuata taratibu za mtihani. Mtihani wenyewe nao uanze Machi 7, 2022 hadi Machi 9, 2022.

Wizi wa mitihani ya kitaifa umekuwa ni changamoto kubwa kwa serikali na hasa Wizara ya Elimu. Mwaka baada ya mwingine hutokea visa kadhaa vya wizi wa mitihani, jambo ambalo huhatarisha hadhi ya vyeti vinavyotokana na matokeo ya mitihani hii.

Ingawaje Wizara ya Elimu imejaribu kupunguza kwa kiasi fulani wizi huo, bado kungali na mianya katika usimamizi na utendakazi wa maafisa wasimamizi wa mitihani au shule kadhaa.

Mnamo mwaka jana, Waziri wa Elimu akitangaza kukamilika kwa mtihani wa KCSE alisema kuwa, wasimamizi wapatao 27 wa mitihani walifutwa kazi kutokana na usimamizi mbaya wa shughuli hizo.

Raia wapatao 35 wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu walikamatwa, na simu za mkononi 53 zikanaswa. Hii ni sehemu tu ya juhudi zilizofanywa na wizara hiyo huku kukiwa bado na changamoto zaidi.

Mwaka huu, kunafaa kuwe na ulinzi na uangalifu zaidi kwani kuna mabadiliko makubwa katika usimamizi wa mitihani yenyewe.

Kinyume na hapo awali, mwaka huu kuna muungano wa shule nyingi ambazo hazikuweza kufikisha idadi ya wanafunzi 30 kama ilivyotangaza Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini (KNEC).

Ni matumaini ya kila Mkenya kwamba, shughuli za mtihani zitaendelea vyema mpaka mwisho bila wizi wowote kutokea ama visa vya utovu wa nidhamu.