WANDERI KAMAU: Wakati umewadia kutetea makundi yanayobaguliwa
Na WANDERI KAMAU
DUNIA inapoendelea kukumbwa na mabadiliko mengi, hasa katika masuala ya kitamaduni, baadhi ya mabadiliko hayo ibuka yamezua mgongano mkubwa wa kitamaduni miongoni mwa jamii za Kiafrika.
Kama kawaida, kuna makundi yanayoshikilia kuwa mchipuko huo wa tamaduni ibuka unalenga kuzipotosha jamii, kwa kuleta mitindo ya kimaisha ambayo kamwe hailandani na Uafrika halisi.
Vivyo hivyo, kuna makundi yenye mitazamo kinzani—yanayosema lazima Afrika iwe tayari kukumbatia tamaduni hizo mpya “ili kuwiana na dunia ya kisasa.”Je, kati ya makundi hayo mawili kinzani, ni nani mkweli na ni yupi anayeipotosha jamii?
Miongoni mwa “mitindo mipya ya kimaisha” ambayo imeibuka ni utata kuhusu nafasi ya watu au ndoa za jinsia moja katika jamii za Kiafrika.
Mwanzoni, hili ni suala lililoonekana kuwa la jamii za Magharibi na ambalo kamwe halingetokea Afrika hata kidogo.
Lilionekana “kumilikiwa” na Wazungu, hivyo ingekuwa vigumu sana kwake kufika Afrika, licha ya mwingiliano mkubwa ambao huwepo kati ya Wazungu na Waafrika. Hata hivyo, ni wazi kuwa mtindo huu umepanuka na kusambaa kote kote duniani—hata Afrika kwenyewe!
Awali, mashoga wengi walikuwa wakiogopa kujitokeza wazi kutangaza hali zao kwa hofu ya kutengwa na jamii. Wengi waliishi maisha ya kisiri, wakifanya lolote wawezalo kutogundulika.
Lakini hali imebadilika. Katika nchi kama Amerika na Uingereza, tayari mabunge ya mataifa hayo yamepitisha sheria za kuwatambua watu hao na kulinda haki zao.Baadhi ya nchi za Afrika kama Afrika Kusini na Botswana pia zimebuni sheria zinazowatambua watu hao.
Kenya, bado kuna hali ya mivutano ya kichinichini baina ya serikali, jamii na taasisi husika kwa jumla, ikiwa watu hao wanapaswa kutambuliwa kisheria au la.
Kinaya ni kuwa, wakati mivutano hiyo inaendelea, baadhi ya Wakenya wamejitokeza wazi na kutangaza kuwa mashoga. Miongoni mwao ni marehemu Binyavanga Wainaina, aliyekuwa kati ya waandishi maarufu zaidi nchini.
Hata hivyo, wakati umefika tukubali kuwa watu hao wapo miongoni mwetu, ambapo lazima tubuni mazingira yatakayowawezesha kuishi maisha yao ya kawaida bila hofu yoyote.
Ingawa hili halilengi kuishinikiza jamii kukumbatia mtindo huo wa kimaisha, inafika wakati ambapo hatuwezi kukana uhalisia ulio nasi katika mazingira tunayokaa.
[email protected]
Next article
Mwanafunzi ajitosa kwa siasa za useneta wa Kilifi