Connect with us

General News

Magavana saba wajishusha bei – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Magavana saba wajishusha bei – Taifa Leo

Magavana saba wajishusha bei

NA CHARLES WASONGA

MAGAVANA saba wamejishusha hadhi kwa kujitosa ulingoni kuwania nyadhifa za useneta na ubunge katika jitihada zao za kusalia katika ulingo wa siasa.

Hii ni baada ya wao kukamilisha mihula yao ya pili na ya mwishoni kwa mujibu wa katiba.

Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Nchi (CoG) Martin Nyaga Wambora, magavana Jackson Mandago (Uasin Gishu), Samuel Tunai (Narok), Ali Roba (Mandera), Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet) na Kivutha Kibwana tayari wameidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kugombea useneta katika kaunti zao.

Naye Gavana Sospeter Ojaamong’ wa Busia ameidhinishwa kuwania kiti cha eneobunge la Teso Kusini, ambalo aliwakilisha bungeni kabla ya kuwa gavana mnamo 2013.

Saba hawa ni miongoni mwa jumla ya magavana 22 ambao hawatatetea viti vyao kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa kuwa katiba haiwaruhusu kushikilia wadhifa huo kwa zaidi ya mihula miwili.

Wadadisi wa masuala ya uongozi na sheria wanasema viti ambavyo magavana hao saba wanagombea ni vya hadhi ya chini.

Hii ndio sababu maseneta Mutula Kilonzo Junior (Makueni), Cleophas Malala (Kakamega), Steve Lelengwe (Samburu), Ephraim Maina (Nyeri), miongoni mwa wengine wanawania ugavana katika kaunti zao kwa kuwa kiti hicho ni kikubwa.

“Kimsingi, kwa kuzingatia kigezo cha ushawishi na fedha, kiti cha useneta ni cha hadhi ya chini kikilinginishwa na ugavana. Kwa hivyo, kwa kuwania useneta wanasiasa hawa wameshuka ngazi,” anasema Barasa Nyukuri.

KUSIMAMIA PESA NYINGI

Bw Nyukuri anaongeza magavana pia husimamia pesa za ziada kama vile ushuru na kodi ambazo serikali zao hukusanya na ruzuku kutoka mashirika mbalimbali ya humu nchini na kimataifa.

Aidha, wakuu hao wa kaunti husimamia, mali na rasilimali za kaunti na wafanyakazi.

“Kwa kusimamia rasilimali kama hizi, magavana huwa ni maafisa wenye ushawishi katika ngazi ya kaunti na kitaifa,” Bw Nyukuri anaeleza.

“Magavana wanaowania ugavana wangefuata mifano ya wenzao, Joho na Oparanya kwa kujipigia debe watengewe vyeo vya uwaziri au hata Makatibu wa Wizara katika mirengo wanazoegemea,” anashauri Wakili Bobby Mkangi.

“Wajibu mkubwa wa maseneta ni kutunga sheria na kutetea ugavi wa fedha katika kaunti na ukaguzi wa matumizi ya fedha katika kaunti, pia ni wenye uzito kiasi,” Bw Mkangi anaongeza.

Lakini Seneta Kilonzo Junior anasema magavana wanaowania useneta na ubunge wanavutiwa na haja ya kufunika maovu waliyotenda katika mihula miwili waliyohudumu.

“Naona kama hao wanataka kufunika ubadhirifu wa fedha na maovu mengine waliyofanya. Hii ni kwa sababu watachambua ripoti za mkaguzi wa hesabu za serikali zitakazoangazia usimamizi mbaya wa fedha katika serikali zao,” akasema seneta huyo.

Hata hivyo, Bw Mandago anakanusha madai hayo akisema atakuwa tayari kuwajibikia matumizi ya fedha katika kaunti yake hata akihudumu kama seneta.

“Haja yangu ni kuendeleza ugatuzi kwa manufaa ya watu wangu wa Uasin Gishu. Wale wanaodai kuwa ninaenda seneta kuficha maovu yangu wanadanganya. Niko tayari kuchunguzwa na asasi za kupambana na ufisadi ikiwa madai ya wizi wa fedha yataibuliwa dhidi yangu,” akasema Bw Mandago.

Nao magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega) na Ali Hassan Joho (Mombasa) wameahidiwa nyadhifa za waziri wa fedha na ardhi mtawalia iwapo mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya utashinda.

Kwa upande wake Gavana wa Migori Okoth Obado ameteuliwa kuongoza kampeni za Kenya Kwanza katika eneo la Nyanza, cheo ambacho kinamweka katika nafasi bora ya kutunukiwa wadhifa mkuu katika serikali endapo Naibu Rais William Ruto atashinda Agosti 9.