Connect with us

General News

Mahakama yatoa agizo NLC itatue zogo la mipaka – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mahakama yatoa agizo NLC itatue zogo la mipaka – Taifa Leo

Mahakama yatoa agizo NLC itatue zogo la mipaka

NA PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA imeagiza kuwa mzozo wa muda mrefu kuhusu mipaka kati ya kaunti za Taita Taveta, Makueni na Kwale utatuliwe na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC).

Mahakama ya Mazingira na Ardhi mjini Mombasa, imemwagiza mwanaharakati Okiya Omtatah kupeleka malalamishi kwa NLC.

Taveta na Makueni zinazozania mji wa Mtito Andei huku Makueni na Kwale zikivutana kuhusu mji wa Mackinnon Road.

Bw Omtatah alikuwa ameelekea mahakamani kutaka agizo litolewe kwa Bunge la Kitaifa na Seneti kubuni tume huru ya kutatua mzozo huo ambao umedumu kwa muda mrefu.

Jaji Lucas Naikuni, ameagiza kwamba ijapokuwa mahakama ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, NLC ndiyo inastahili kushughulikia mzozo uliopo kisha ripoti iwasilishwe kortini.

Wakati uo huo, jaji huyo aliahirisha kusikilizwa kwa kesi hiyo kwa miezi sita ili kumpa nafasi Bw Omtatah kuipeleka kwa NLC.Bw Omtatah alikuwa ameambia mahakama aliwasilisha kesi hiyo kwa niaba ya wakazi wa Taita Taveta.

Jaji Naikuni pia aliagiza Serikali ya Kaunti ya Taita Taveta iwe pekee yenye mamlaka kwa sasa kutoa vibali vya kibiashara na kutoza kodi katika miji ya Mtito Andei na Mackinnon Road.

Taita Taveta iliagizwa kuhifadhi kodi zote zinazokusanywa, kwenye akaunti ya benki inayoleta riba ambayo itafunguliwa kwa pamoja na Kaunti za Kwale na Makueni.

Hata hivyo, Makueni imepinga maagizo hayo ikidai kuwa, Bw Omtatah hakueleza mahakama ukweli na hivyo kuipotosha.