– Wakhungu alishtakiwa pamoja na Mbunge wa Sirisia, John Waluke na kampuni ya Erad Suppliers kwa kutapeli Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) kuwalipa KSh 297 milioni
-Hakimu Mwandamizi Elizabeth Juma alisema Wakhungu ambaye ana miaka 79, amekuwa akichezea mahakama mchezo wa paka na panya na kuchelewesha hukumu
– Wakili wa Wakhungu, Ian Wand aliambia mahakama kuwa mteja wake alilazwa hospitalini mnamo Juni 7 na bado anaugua
– Wakhungu na Waluke Wawili hao wanashtumiwa kuwa mnamo Februari 24, 2009, wakiwa wakurugenzi wa kampuni hiyo, waliwasilisha stakabathi feki kama ushahidi
Mahakama moja jijini Nairobi imetoa idhini ya kukamatwa kwa dada yake makamu wa rais wa zamani Moody Awori, Grace Wakhungu katika kesi ya utapeli wa KSh 297 milioni.
Wakhungu alishtakiwa pamoja na Mbunge wa Sirisia, John Waluke kwa kughushi stabathi za kampuni ya Erad Suppliers katika sakata ya mahindi iliyowashuhudia wakipokea KSh 297 milioni kupitia njia udanganyifu.
Huku akitoa amri hiyo, Hakimu Mwandamizi Elizabeth Juma alisema Wakhungu ambaye ana miaka 79, amekuwa akichezea mahakama mchezo wa paka na panya na kuchelewesha hukumu kutolewa.
“Korti imetambua kuwa mshtakiwa wa kwanza ambaye anasemekana kuugua mshtuko wa moyo anazungusha korti hii. Hii ni mara ya pili kukosekana, sasa ninatoa idhini ya kukamatwa kwake,” aliamuru Juma.
Mbunge wa Sirisia, John Waluke pamoja na Grace Wakhungu walipofikishwa kortini.Picha: Africantimes. co.ke. Source: Facebook
Wakili wa Wakhungu, Ian Wand aliambia mahakama kuwa mteja wake alilazwa mnamo Juni 7, katika Kituo cha Daima Afya Medical, mtaani Gumba na bado anaugua.
Aliwasilisha stakabathi zake za matibabu mbele ya mahakama ili kuthibitisha.
Hata hivyo, hakimu alishikilia kuwa mshtakiwa alitakiwa kufika mbele ya mahakama kujieleza.
Alidokeza kwamba hukumu wa kesi hiyo imekuwa tayari na Wakhungu amekuwa akivuta mahakama nyuma.
“Mshtakiwa wa kwanza angefika hapa na kujieleza. Hukumu imekuwa tayari kwa muda,” alisema hakimu
Kulingana na mashtaka iliyowasilishwa, Wakhungu na Waluke ni wakurugenzi wa Erad Suppliers Ltd, kampuni ambayo wanadaiwa kutumia kufuja KSh 297 milioni katika kandarasi kati yao na Chelsea Freight na Halmashauri ya Nafaka na Mazao (NCPB) .
Wawili hao wanashtumiwa kuwa mnamo Februari 24, 2009, wakiwa wakurugenzi wa kampuni hiyo, waliwasilisha stakabathi feki ya kuonyesha ushahidi ya tofauti zao na NCPB.