General News
Mambo kwa ‘ground’ si mzaha, Wakenya wanateswa na Covid – Taifa Leo
Published
4 years agoon
By
Taifa Leo [ad_1]
Na SAMMY WAWERU
KWENYE nyumba ya Dickson Muceri yenye ukubwa wa mita 8 kwa 10, eneo la Fountain Junior katika mtaa wa Githurai 45, kiungani mwa jiji la Nairobi, unapoingia utakaribishwa na godoro, stovu ya kupika inayotumia mafuta ya taa, vifaa kadha vya mapishi na beseni.
Mazingira aliyomo yamechangiwa na janga la Covid-19, ambalo likitajwa kusaga uchumi anahisi makali yake.
Muceri, 38, ni mume na baba wa mtoto mmoja na hivi karibuni anatarajia kujaaliwa wa pili.
Kabla kujipata katika hali hiyo, anasema alikuwa ameinuka kimaisha na kimaendeleo, kiasi cha kumudu kununua tuktuk, aliyokuwa amewekeza katika sekta ya usafiri na uchukuzi Githurai.
Mfanyabiashara huyu alikuwa ameweka mikakati kibao kujiboresha, kutokana na kazi ilivyonoga.
Miezi kadha baada ya Machi 2020 maisha yalianza kuchukua dira tofauti. Visa vya maambukizi ya corona vilivyozidi kuongezeka na kanuni zilizowekwa kusaidia kuzuia msambao, ndivyo mambo yaliharibika.
“Awali, nilikuwa natia kibindoni mapato yasiyopungua Sh1,500 kwa siku. Covid-19 iliyashusha hadi chini ya Sh1, 000. Gharama ya mafuta na matumizi mengine barabarani ikiondolewa, kilichosalia kisingetosha kukidhi familia yangu kimapato,” Muceri anaeleza.
Kuuza jembe la kazi
Amri ya matatu kubeba asilimia 60 ya idadi jumla ya abiria na pia kafyu, ikawa kichocheo cha biashara kuzorota.
“Nyakati nyingine ningepeleka nyumbani Sh100 pekee, hasa gari linapopata hitilafu. Ni kazi ya juakali, ambayo ni vigumu kutabiri kiwango cha mapato, mke asingeelewa,” anasimulia, akifichua kwamba hatua hiyo ilianza kuzua mizozano ya kifamilia.
Hatimaye, kilele kikawa kuuza jembe lake la kazi Desemba 2020. Kwa mujibu wa masimulizi yake kilichochochea hilo, ni swali alilomuuliza mkewe: “Ikiwa umeshindwa kukimu familia riziki nieleze wazi.”
Lilimuuma moyo, na kwa sababu ya mapenzi aliyonayo kwa familia yake changa hakuwa na budi ila kuinusuru.
“Ilikuwa vigumu kumshawishi mambo yalivyokuwa nyanjani, kwa kuwa aliona nikiamkia kibarua alfajiri na mapema na kurejea usiku, alishangaa yalikoenda mapato. Niliuza tuktuk yangu kwa bei ya hasara, nikaenda mashambani ninakotoka, eneo la Chuka, Kaunti ya Tharaka Nithi, nikakamilisha ujenzi wa nyumba yangu na kuhamishia familia humo mwanzoni mwa 2021,” anafafanua.
Shughuli hiyo ilikuwa gharama, iliyomlazimu kufukua mfuko zaidi na kusafirisha vifaa vya kuanza upya maisha mashambani.
Anasema alichukua hatua hiyo kwa sababu ya gharama nafuu mashambani, hususan kuwepo kwa chakula cha kutosha, uamuzi ambao umechukuliwa na wengi waliolemewa baada ya kufutwa kazi.
Msongo wa mawazo ukionekana kumlemea, kwa sasa tegemeo lake ni vibarua vya kuendesha tuktuk na anavyohoji havipatikani, angalau aweze kumshughulikia mke wake anayetarajia kujifungua wakati wowote. Mbali na sekta ya usafiri na uchukuzi, zingine zilizoathirika zaidi ni pamoja na utalii, hoteli, elimu, kati ya nyinginezo, mamia, maelfu na mamilioni ya wafanyakazi wakipoteza ajira.
Kulingana na takwimu za serikali, zaidi ya watu milioni 1.72 wamepoteza ajira kutokana na athari za corona.
Baadhi ya wamiliki wa biashara, hasa katika sekta ya hoteli waliishia kukunja jamvi utoaji huduma, wenye shule za kibinafsi wakigeuza madarasa kuwa vizimba vya kuku na uwanja uga wa kilimo.
Simulizi na mahangaiko ya Dickson Muceri si tofauti na ya Lucy Mukami, 28, mkazi wa eneo la Maziwa, Kahawa West, Nairobi.

Mukami ni mama wa watoto wawili, kifungua mimba mwenye umri wa miaka 14 na yule mdogo miaka 5.
Alikuwa katika sekta ya hoteli, na ambayo inaendelea kuyumbishwa na athari za corona.
“Kuanzia Agosti 2020 sijakuwa kazini, nimekuwa nikitegemea vibarua vya kufulia watu nguo,” Mukami akasema kwenye mahojiano.
Huku mapato yake kupitia vibarua anavyopata akikadiria kuwa kati ya Sh800 – 1, 500 kila juma, mama huyo ana wasiwasi atakavyoweza kulipia wanawe karo shule zitakapofunguliwa wiki ijayo.
“Shuleni anakosomea binti yangu, ninadaiwa malimbikizi ya karo ya Sh12,000. Mambo yanazidi kuwa magumu,” anasema.
Katika eneo la Zimmerman, Nairobi, Dennis Kinyua ni mkazi mwingine ambaye anaendelea kuteswa na makali ya janga hili.
Ni mhudumu wa muda wa mkahawa mmoja eneo la Juja, Kaunti ya Kiambu, mapato anayopokea akisema ni ya kulipa kodi ya nyumba.
“Kwa mwezi ninalipwa Sh6, 000, mapato hayo nikiondoa gharama ya nauli ninasalia na pesa za kulipa kodi ya nyumba pekee. Isitoshe, ninaenda kazini siku mbili au tatu kwa wiki. Ninadaiwa kodi ya miezi miwili,” Kinyua anafafanua, akishangaa atakavyomudu maisha endapo serikali haitaweka mikakati faafu kuokoa wananchi.
Dhuluma za kijinsia
Masimulizi ya tuliozungumza nao yakiashiria matatizo ambayo Wakenya walioathirika wanapitia, visa vya ‘talaka’, dhuluma za kijinsia (GBV) katika familia na pia baadhi kutekeleza mauaji kutokana na hali ngumu ya kimaisha na kiuchumi vimeripotiwa.
Wengine wajitia kitanzi
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Utumishi wa Umma, Jinsia na Masuala ya Vijana, visa 5, 009 vya dhuluma za kijinsia viliandikishwa kati ya Januari 2020 – Desemba 2020, kupitia nambari maalum ya 1195.
Huku Come Together Widows and Orphans Organization (CTWOO), shirika lilisilo la kiserikali na linaloangazia masuala ya wajane na yatima, likiandikisha zaidi ya malalamishi 150 ya GBV kutoka kwa wanawake walio kwenye ndoa, tangu Machi 2020, linakiri hali ngumu ya maisha na kiuchumi inayochochewa na Covid-19 imechangia ongezeko la vita vya kijinsia.
“Hali ni mbaya zaidi kiasi cha kuwa baadhi ya kina mama wanajitolea kutoa watoto wao kwa wanaojiweza, ili wasife njaa. Nimepokea visa viwili vya aina hiyo,” Dianah Kamande HSC, mwanzilishi na Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika hilo akaambia Taifa Leo wakati wa mahojiano.
“Mfano, ratiba yangu ya mwezi huu wa Aprili ina matukio chungu nzima kusambaza chakula, nimepokea visa vya maelfu ya wanaohangaika kupata angaa cha kutia tumboni. Ninahimiza wasamaria wema tuungane kusaidia Wakenya wenzetu,” Dianah akaomba.
Tangu virusi vya corona vikite kambi nchini, CTWOO pia imeandikisha zaidi ya visa 1, 800 vya GBV miongoni mwa wajane, baadhi wakiwa wahasiriwa waliolemewa na athari za janga hili.
Hofu ya afisa wa polisi anayeangazia GBV
Ni ongezeko la visa vya dhuluma za kijinsia linalomtia hofu Caroline Njuguna, Afisa wa Idara ya Polisi na ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuangazia GBV.
Afisa huyo mwenye ngazi ya cheo cha Inspekta Mkuu, ni mwasisi na mlezi wa Shirika la Kijamii la Boots and Brains Initiative, linaloangazia visa vya dhuluma za kijinsia nchini.
“Nina wasiwasi jinsi familia nyingi zimeathirika, visa vya GBV vimepanda zaidi ya mara dufu. Hatua hiyo inatatiza ukuaji wa watoto, na huenda siku za usoni watapotoka kimaadili na wengine kuchukia ndoa,” anaonya Caroline ambaye pia ni mshauri nasaha na mpatanishi wa familia.
Chini ya mradi wake aliouanzisha 2018, kipindi hiki cha Covid-19 afisa huyo amekuwa akijituma kuwapa chakula na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi wasiojiweza katika jamii.
Kwa Dickson Muceri na ambaye aliamua kuipeleka familia yake mashambani kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi jijini, ni dua kwa Mwenyezi Mungu aweze kumjalia milango ya heri.
Hata hivyo, kinachomkwaza zaidi ni kuona serikali ikiupa kipaumbele Mswada wa Ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI), kipindi ambacho yeye na wahasiriwa wengine wanaendelea kuhangaika, badala ya kukwamua uchumi.
[ad_2]
Source link
Comments
You may like
Rayvanny officially leaves Diamond’s WCB Wasafi after 6 years

Raila Odinga is the most popular presidential candidate, a survey released by Infotrak

Newly-crowned Kenyan Wimbledon champion Angella Okutoyi would like to play against American star Serena Williams

The Mombasa High Court has ordered IEBC to clear Sonko to run for the Mombasa governorship.

A new born baby was pulled out of latrine in Mururi.

Kenyan Rapper Colonel Mustafa has leveled fresh accusations against his ex-girlfriend Katoto.

Okutoyi and Nijkamp qualify for Wimbledon Open final

Fans will have to brace themselves for a sober 90 minutes, the Gulf Arab state announces.

Angola’s longest ruler dos Santos dies at 79
