WANDERI KAMAU: Manifesto zimegeuzwa jukwaa za kupotosha raia
Na WANDERI KAMAU
MANIFESTO huwa ni orodha ya ahadi za kisiasa, kiuchumi na kijamii ambazo vyama ama wagombea wa nyadhifa mbalimbali huahidi kuwatimizia wafuasi wao ikiwa watafaulu kutwaa nafasi hizo.
Ni mtindo ambao umekuwepo kwa muda mrefu katika mifumo yote ya kiutawala ambayo ishawahi kuwa hapa duniani—ya kidemokrasia, kifalme ama kikomunisti.
Chimbuko lake lilitokea katika jamii za kale barani Asia—hasa Ugiriki—ambako ndiko mfumo wa utawala wa kidemokrasia ulianza.
Baadaye, matumizi yake yalisambaa kote duniani, kiasi cha wasomi kuandika vitabu na majarida mengi kurejelea chimbuko na maana yake halisi.
Miongoni mwa wasomi hao ni Karl Marx na Friendrich Engels, walioandika kijitabu ‘The Communist Manifesto’ (Manifesto ya Kikomunisti) mnamo 1896, kuwasaidia watawala duniani kurejelea mbinu za kisiasa wanazopaswa kutumia ili kuboresha tawala zao.
Ingawa ni kijitabu kidogo, moja ya ushauri wake mkuu kwa wanasiasa ni kwamba wanapaswa kutoa ahadi ambazo wanaweza kuzitimiza.
Wasomi hao wanasema ni kosa kubwa la kisiasa kwa kiongozi yeyote kutoa ahadi ambazo ni vigumu kuzitimiza, kwani atakuwa kama “wakala wa uwongo.”
Sababu kuu ya urejeleo huu ni ahadi ambazo zimekuwa zikitolewa na vigogo mbalimbali wanaolenga kuwania nyadhifa tofauti za kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Wale wanaotazamwa sana ni Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga (aliyezindua azma yake ya urais Ijumaa iliyopita), Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu) kati ya wengine.
Ingawa hajazindua rasmi manifesto yake, Dkt Ruto amesema moja ya masuala atakayoshughulikia zaidi ikiwa atachaguliwa kuwa rais, ni kuboresha uchumi kupitia mpango wa kuwapa wananchi mikopo midogo kujiinua kimaisha, maarufu kama “Bottom up.”
Ili kufanikisha mpango huo, amesema serikali yake itatenga Sh100 bilioni katika miezi mitatu ya kwanza ya utawala wake kumwezesha kutimiza ahadi hiyo.
Alipotangaza azma yake ya urais Ijumaa, Bw Odinga alizua msisimko miongoni mwa wafuasi wake, aliposema kuwa serikali yake itakuwa ikitioa msaada wa Sh6,000 kila mwezi kwa familia karibu milioni mbili nchini ambazo jamaa zao hawana ajira rasmi.
Katika nchi zilizostawi kidemokrasia kama Amerika na Ujerumani, manifesto huwa zinatolewa na vyama vya kisiasa badala ya wawaniaji binafsi.
Hata hivyo, hali ni tofauti hapa nchini, kwani wanasiasa hutoa manifesto hivyo tu bila kuzingatia uwezo wao kuzitimiza wala hali ya kiuchumi nchini.
Hilo ndilo limezifanya nyingi kuwa jukwaa tu la wanasiasa kuwapumbaza wananchi bila kujali ikiwa watazitimiza au la.
Wakenya wafunguke macho!
[email protected]