VALENTINE OBARA: Mashambulio yazimwe kabla kuenea kwingine
NA VALENTINE OBARA
KWA wiki ya pili sasa, sehemu kadha za Kaunti ya Lamu zimekuwa hazikaliki kwa sababu ya mashambulio yanayosababisha maafa.
Ijapokuwa serikali haijaeleza wazi chanzo cha mashambulio hayo, dalili tofauti zinaashiria uwezekano kuwa yanatekelezwa na magaidi.
Maafisa serikalini wangali wanasubiriwa kubainishia umma ikiwa kweli ni magaidi wanahusika au ni mizozo ya ardhi inavyodaiwa na baadhi ya viongozi, au kuna uchochezi wa kisiasa unaohusiana na uchaguzi ujao.
Ikizingatiwa mtindo ambao magaidi wamekuwa wakitumia tangu zamani, uwezekano kuwa hivi ni vitendo vyao kabla watekeleze shambulio kwingine ndani ya nchi haufai kupuuzwa hata tunaposubiri chanzo halisi cha mashambulio kubainishwa.
Itakumbukwa kuwa, wakati ulimwengu ulipokuwa ukijiandaa kualika mwaka mpya wa 2022, serikali ya Uingereza ilitoa ilani kwa raia wake kuhusu uwezekano wa mashambulio ya kigaidi humu nchini.
Ilani hiyo iliwataka raia wa Uingereza kuwa waangalifu wanaposafiri humu nchini hasa katika sehemu ambazo watu wengi hukusanyika kama vile maabadani, majengo ya kibiashara na maeneo ya burudani.
Hata hivyo, hali ya usalama katika sehemu za Lamu haijakuwa shwari kwa muda mrefu kutokana na kuwa eneo hilo limepakana na Somalia ambapo ni ngome ya kundi la wapiganaji wa Al-Shabaab.
Hii ni mojawapo ya sababu ambazo zimepelekea Jeshi la Ulinzi wa Taifa (KDF) liendelee na operesheni ya kiusalama katika msitu wa Boni.
Lamu ni baina ya maeneo ya nchi ambapo mashambulio ya kigaidi yamekuwa yakiendelea kutokea licha ya kuwa asasi za kiusalama zilifanikiwa kuzima mashambulio katika miji mingine ndani ya nchi.
Eneo hilo ni miongoni mwa yale ambayo Uingereza na nchi nyingine za nje huonya raia wao kuwa waangalifu kila wanapotembelea kwa takriban mwongo mmoja sasa.
Huenda mashambulio yanayotokea sasa yakahusishwa na mizozo ya ardhi au uchochezi wa kisiasa ila hiyo pia ni mitindo ambayo magaidi wamekuwa wakitumia tangu zamani.
Ni bayana kuwa makundi ya kigaidi yanaposhindwa katika ajenda zao za kishetani, huwa wanageukia mbinu za kujaribu kugawanya nchi au kusambaratisha uchumi wake.
Tunapokuwa katika mwaka wa uchaguzi, tuwe waangalifu tusije tukatumbukia kwa malengo ya magaidi ambao huenda wakataka kutumia mihemko ya kisiasa kuleta makabiliano ya kikabila dhidi ya jamii tofauti wanaposhambulia jamii moja katika eneo la nchi.
Jaribio lao la awali kuleta ghasia kwa msingi wa kidini katika taifa hili hazikufua dafu, na jaribio la kuingilia tofauti zetu za kikabila pia halifai kupewa nafasi.
Asasi za usalama wa taifa zinastahili kukaza kamba kuzima matukio hayo na kulinda uchumi wa Lamu na taifa zima hasa ikizingatiwa miradi mikubwa ambayo serikali iliwekeza katika eneo hilo.
Miradi kama vile ya bandari ya Lamu ambayo tayari imeanza shughuli zake, huenda ikaathirika vibaya ikiwa mashambulio yataendelea kuhangaisha nchi kwa maafa na uharibifu wa mali.
Raia watakaopatikana kuficha wahalifu hao pia wachukuliwe hatua kali.
Next article
KINYUA BIN KING’ORI: Wanasiasa sharti wachague kwa…