Connect with us

General News

Maswali tele kuhusu Kadhi Mkuu kustaafu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Maswali tele kuhusu Kadhi Mkuu kustaafu – Taifa Leo

Maswali tele kuhusu Kadhi Mkuu kustaafu

NA FARHIYA HUSSEIN

HALI ya suintofahamu imeibuka miongoni mwa baadhi ya Waislamu kuhusu kustaafu kwa Kadhi Mkuu Ahmed Muhdhar.

Sheikh Muhdhar ambaye alitarajiwa na wengi kustaafu Novemba mwaka uliopita, sasa amesema kipindi chake hakijakamilika.

Katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Sheikh Muhdhar alisema bado yuko ofisini hadi Novemba mwaka huu.

“Bado natumikia Ofisi ya Kadhi. Si – kutakiwa kustaafu mwaka jana bali mwisho wa Novemba mwaka huu,” alisema.

Mwaka uliopita, kulikuwa na midahalo mikali miongoni mwa waumini wa dini ya Kiislamu kuhusu urithi wa kiti hicho cha Kadhi Mkuu kwa matarajio kwamba kipindi chake cha kuhudumu, kilifaa kukamilika.

Hata hivyo, mwezi Novemba ulipita na hatimaye mwaka ukakamilika bila mipango yoyote kuonekana kuchukuliwa kutafuta Kadhi Mkuu mpya.

Mnamo Machi mwaka uliopita, Sheikh Muhdhar ambaye ni Kadhi Mkuu wa kwanza chini ya Katiba ya Kenya iliyopitishwa mwaka wa 2010, alisema alikuwa tayari kuondoka ofisini bila majuto kwa vile anaamini amefanya kazi zake zote ipasavyo.

Hata hivyo, ameeleza kuwa pindi atakapokuwa nje ya mamlaka ndipo Tume ya Huduma za Mahakama (JSC), itatangaza tarehe za zoezi la uteuzi wa Kadhi Mkuu mpya.

“Mchakato wa siku hizi unahusisha kutangaza nafasi. Ni watu wenye sifa stahiki pekee wanaoweza kuwa Kadhi Mkuu. Nafasi hiyo inaweza kuchukuliwa na mtu kutoka sehemu yoyote ya nchi. Si lazima kutoka Pwani,” akasema.

Sheikh Muhdhar amehudumu kwa miaka 11 kama Kadhi Mkuu. Duru ziliambia Taifa Leo kuwa, muda anaoendelea kutumikia uliongezwa kufuatia mijadala mikali iliyoibuka kuhusu uteuzi mwaka jana.

Mratibu wa Baraza Kuu la Waislamu, (SUPKEM), Pwani, Bw Khamis Mwaguzo, alithibitisha kuwa kulikuwa na mijadala mingi ambayo iliibuka kuhusu wadhifa huo.

“Kulikuwa na mjadala mkubwa uliokuwa ukiendelea kuhusu njia ya uteuzi iliyotumika. Maombi na njia za mchujo zilileta mjadala mkali,” alisema katika mahojiano jana.

Baadhi ya masuala yaliyoibuka ni kutaka wadhifa huo ushikiliwe kwa mzunguko kutoka ukanda mmoja wa nchi hadi mwingine, ili isionekane kwamba ni wadhifa wa Muislamu mwenye asili ya Pwani pekee.

Vile vile, wanawake wasomi Waislamu pia waliibua suala la kutaka wazingatiwe katika nyadhifa zilizo katika Mahakama ya Kadhi, wakisema wale walio miongoni mwao hasa waliosomea sheria, wana uwezo wa kutumikia.

Kulingana nao, kuna masuala mengi ambayo wanawake wanaohitaji huduma katika Mahakama za Kadhi huwa wanaogopa kueleza wanaume, kwa hivyo kunafaa kuwe na nafasi za wanawake wanaoweza kuwahudumia.

Katika mahojiano ya awali, Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Ushauri la Waislamu Kenya (Kemnac), Sheikh Juma Ngao, alikuwa ameitaka JSC kushirikisha umma inapoendesha zoezi la kutafuta Kadhi Mkuu mpya.

“Safari hii tunataka wananchi wapewe nafasi ya kufuatilia shughuli nzima. Kuanzia kwenye mchujo hadi kuapishwa kwa Kadhi. Iwe ni nafasi za Kadhi Mkazi au Kadhi Mkuu wa Kenya,” alisema Sheikh Ngao.

Alibainisha kuwa jinsi maafisa mbalimbali wa kiserikali hufanyiwa mahojiano yanayopeperushwa moja kwa moja kwenye runinga, pia wale wanaowania nyadhifa za Kadhi , wanapaswa kufanywa kwa njia hiyo hiyo ili kuwe na hakikisho kuwa wanaoteuliwa ni watu waliohitimu.

Wakati huo huo, Sheikh Ngao alisema wataalamu wa kisheria wa dini ya Kiislamu wamepanga kukongamana wiki ijayo ili kujadiliana kuhusu uwezekano wa kuwa na muungano mmoja wa Waislamu.