[ad_1]
Matiang’i aonya wanasiasa wenye ndimi za moto
NA WYCLIFFE NYABERI
WAZIRI wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i amesema serikali haitamsaza mwanasiasa yeyote atakayewachochea Wakenya kuzua rabsha uchaguzi mkuu wa Agosti unapokaribia.
Badala yake, Dkt Matiang’i amewataka wanaomezea mate viti mbali mbali, kunyenyekea na kutafuta kura zao kiustaarabu bila kuwagonganisha na kuwagawanya Wakenya ambao wameishi kwa umoja muda mrefu.
Akiongea Ijumaa alipozuru kijiji cha Endiba, eneobunge la Borabu kaunti ya Nyamira, alikozindua kisima cha maji kwa wakazi hao, waziri alisema kipindi hiki taifa hili linapojiandaa kwa uchaguzi, wanasiasa wanafaa kuwa waangalifu kuepuka malumbano, matusi na chuki dhidi yao.
Wale watakaowatumia Wakenya kusambaratisha juhudi za amani ambazo serikali imeweka kulingana na Dkt Matiang’i watachukuliwa hatua kali.
“Hatutakubali yeyote asambaratishe juhudi za serikali kwa kuwagonganisha watu wetu. Kila mmoja apewe nafasi ya kuuza sera zake na nyinyi wenyewe mtaamua ni nani anayefaa,” Dkt Matiang’i akasema.
Semi kama hizo zilitolewa na Mshirikishi wa Serikali eneo la Nyanza Bw Magu Mutindika. Afisa huyo alisema wameweka juhudi za kutosha kwa wakazi wa Nyanza kuishi kwa amani. Aliwatahadharisha wanasiasa wanaopenda kuwadhihaki wenzao.
Kama ilivyo kawaida yake, Dkt Matiang’i aliiomba jamii ya Abagusii izidi kuishi pamoja na kuwaheshimu viongozi wao.
Kuhusu siasa za kitaifa, waziri alidokeza atazidi kuchukua mwelekeo unaochukuliwa na mkubwa wake Rais Uhuru Kenyatta.
Alimshukuru kiongozi wa taifa kwa nafasi aliyompa kuhudumu serikalini na kutaja kuwa wadhfa aliompa ni ishara nzuri kuwa anaipenda jamii yake.
Baada ya hafla hiyo, Dkt Matiang’i alijumuika na Inspekta Generali wa polisi Hillary Mutyambai kufungua majengo ya kituo cha polisi cha Matutu.
[ad_2]
Source link