#KCPE2021: Matokeo ya Kiswahili yaimarika
Na CHARLES WASONGA
KISWAHILI ni miongoni mwa masomo sita ambayo matokeo yake yaliimarika katika mtihani wa kitaifa wa darasa nane (KCPE) 2021 ikilinganishwa na mwaka wa 2020.
Watahiniwa hasa waliandikisha matokeo mazuri katika karatasi ya Kiswahili Lugha na Kiswahili Insha, kulingana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha.
“Aidha, nina fuhara kutangaza kuwa wanafunzi pia walifanya vizuri katika insha ya Kiingereza, Insha ya Lugha ya Ishara, Sayansi na Somo la Kijamii ikilinganishwa na matokeo ya mwaka wa 2020,” Prof Magoha akasema alipotangaza rasmi matokeo ya mtihani huo katika makao makuu ya Baraza la Mitihani (KNEC), jumba la Mitihani, Nairobi.
Hata hivyo, matokeo katika masomo ya Hisabati, Lugha ya Kiingereza na Dini yalishuka katika mtihani wa 2021 ikilinganishwa na mwaka wa 2020.
“Hata hivyo, matokeo katika Lugha ya Ishara yalikuwa sawa na ilivyokuwa mwaka wa 2020,” Prof Magoha akaeleza.
Kwa misingi ya jinsia, watahiniwa wa kiume na kike waliandikisha matokeo yanayokaribiana. Hata hivyo, wasichana walifanya vizuri kuliko wavulana katika masomo ya Kiswahili na Kiingereza.
“Wavulana nao walifanya vizuri, japo kwa kiwango kidogo, kuliko wenzao wasichana, katika Lugha ya Ishara ya Kenya, Hisabati, Sayansi, Sayansi Jamii na Elimu ya Dini,” Prof Magoha akaeleza.
Kwa jumla matokeo ya KCPE ya 2021 yalikuwa mazuri ikilinganishwa na matokeo ya mwaka wa 2020.Hii ni licha ya mtahiniwa aliyepata alama ya juu zaidi 2020, Mumo Faith ( 433) kumshinda Magata Bruce aliyeongoza 2021 (428)
.“Hata hivyo, alama ya wastani na gredi za watahiniwa wote 2021 ni juu ikilinganishwa na 2020. Kwa mfano, watahiniwa 8,091 (asilimia 0.68%) walipata kati ya alama 400 na 500 katika KCPE 2020, idadi hiyo imeongezeka hadi 11,857 (asilimia 0.97) katika matokeo ya KCPE 2021,” Prof Magoha akaeleza.
“Hii ni ishara tosha kwamba watahiniwa walipata alama bora kuliko mwaka uliotangulia,” akaongeza huku akiwapongeza walikuwa waliowaandaa watahiniwa hao 1,214,031 katika mazingira magumu.
Next article
#KCPE2021: Waliojaribu kuiba mtihani kuadhibiwa