KPA: Mbinu mpya ya ajira yapingwa kortini
NA BRIAN OCHARO
MAMLAKA ya Bandari za Kenya (KPA) imeshtakiwa kwa madai ya kutumia mbinu haramu ya kuajiri wafanyakazi.
Hii ni baada ya wafanyakazi 38 kuajiriwa kupitia kwa mbinu hiyo mpya huku wengine wakipandishwa vyeo.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Genesis For Human Rights Commission (GHRC), limepinga hatua ya KPA kufanya mabadiliko katika sera zake za ajira.
Shirika hilo limedai kuwa, hatua hiyo haikufuata sheria na utekelezaji wake utakiuka haki za wafanyakazi na wananchi wengine wanaotazamia kuajiriwa na KPA katika siku za usoni.
Vile vile, shirika hilo limekosoa KPA likidai haikujumuisha maoni ya umma kabla ya kuunda na kuanza kutumia sera hiyo hivyo basi kunyima utaratibu huo uhalali na uaminifu.
“Mlalamishi anahofia kwamba ukiukaji unaotekelezwa na KPA utaendelea bila kudhibitiwa, mtindo utawekwa ambapo sheria na taratibu za kutunga sera katika taasisi za umma zitafanywa kinyume na sheria,” akasema Mkurugenzi wa shirika hilo, Bw Caleb Ng’wena.
Zaidi ya hayo, GHRC imehoji maamuzi ya Waziri wa Fedha Ukur Yatani kuidhinisha sera hiyo iliyorekebishwa ikizingatiwa kuwa hana mamlaka ya kufanya hivyo.
Kulingana na shirika hilo, Mkuu wa Utumishi wa Umma ndiye amepewa mamlaka ya kisheria kutoa idhini yoyote aina hiyo kwa taasisi za umma ikiwa ni pamoja na kurekebisha sera kuhusu mashirika ya serikali.
“Kwa hivyo, barua ya Waziri Yatani (kuidhinisha sera hiyo) haina msingi,” akasema Bw Ng’wena.
Shirika hilo linadai kuwa barua hiyo ya Bw Yatani inatoa idhini ya masharti kulingana na tathmini itakayofanywa na KPA ili kubaini kiwango cha manufaa ya mpango wa matibabu kwa watakaoajiriwa katika taasisi hiyo.
Kulingana na hati zilizowasilishwa mbele ya Mahakama ya Ajira mjini Mombasa, KPA kupitia Mkutano Maalum wa Bodi ilizingatia na kuidhinisha uteuzi wa wafanyikazi 38 kwa kutumia mtindo huo mpya baada ya kupokea barua kutoka kwa waziri huyo.
“Matokeo ya mkutano wa bodi hiyo ni kwamba wafanyakazi wachache walinufaika kutokana na mchakato wa kiubaguzi uliojiri kwa njia isiyostahili kwa kutozingatia tamaduni ya kuajiri na kuwapandisha watu vyeo katika taasisi hiyo,” Bw Ng’wena alisema.
Anaendelea kudai kuwa kutokana na mabadiliko ya sera hizo, ajira kadhaa zimepeanwa katika taasisi hiyo kinyume na sheria.
Bw Ng’wena pia anaitaka mahakama kufutilia mbali utekelezaji wa mapendekezo hayo na kusimamisha kwa muda kuajiriwa kwa watu hao 38.
Jaji Byram Ongaya ameidhinisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuelekeza Bw Ng’wena kuwapa washtakiwa hati za mashtaka.Jaji huyo pia amemruhusu Bw Ng’wena kuanzisha kesi ya kupinga marekebisho hayo.
“Ombi la kutaka kuajiriwa kwa wafanyikazi 38 kusimamishwe, limekataliwa kwa sasa,” alisema Jaji Ongaya.
Bw Ng’wena ameshtaki KPA, Wizara ya Fedha na ile ya Uchukuzi. Tume ya Utumishi wa Umma imeorodheshwa kama mhusika katika kesi hiyo.
Next article
Wagombea urais 55 wahatarisha uchaguzi