PATA USHAURI WA DKT FLO: Mbona mkojo wangu hauishi?
Mpendwa Daktari,
MIMI ni mwanamume. Kwa kawaida mimi hunywa kama lita mbili za maji kila siku ila mkojo wangu ambao huwa mwangavu hutiririka kwenye nguo zangu za ndani; huvunda.
Kwa kawaida mimi huchutama ninapokojoa lakini ninapoamka na kwenda kukaa, nahisi mkojo ukitiririka. Mimi hutingisha uume wangu ilhali nahisi kana kwamba mkojo umesalia.
Mimi hula chakula cha kawaida na sinywi pombe wala kutumia mihadarati, na sina maradhi ya zinaa. Je tatizo laweza kuwa nini?
Charlie, Nairobi
Mpendwa Charlie,
Kwa kawaida mkojo huwa na harufu ya ammonia. Harufu hii huwa na nguvu au hafifu kuambatana na kiwango cha maji ulichokunywa. Harufu ya mkojo yaweza athiriwa na vyakula na vinywaji (kwa mfano vitunguu, vitunguu saumu, virutubishi, pombe, na kahawa), dawa na vijalizo vya vitamini. Maradhi ya kisukari pia yaweza athiri harufu ya mkojo. Kuna maradhi ya kijinetiki kama Maple syrup urine disease na phenylketonuria ambayo yaweza athiri harufu ya mkojo, lakini huwa adimu sana na hutambulika utotoni. Endelea kunywa maji kwa wingi na uepuke vyakula na vinywaji ambavyo vyaweza athiri harufu ya mkojo. Tatizo la kutiririka kwa mkojo baada ya kukojoa linajulikana kama post micturition dribble. Hali hii huwakumba wanaume wengi kwa sababu wakati wa kukojoa, mrija unaopitisha mkojo (urethra), kwa kawaida hujipinda, na huenda mkojo kidogo ukasalia ndani na kutiririka baadaye. Njia ya kipekee ya kukabiliana na tatizo hili ni kujipa muda unapokojoa ili mkojo uliosalia utiririke.Aidha, fanya mazoezi ya nyonga ili misuli ya sehemu hii iwe thabiti na iweze kusukuma mkojo nje. Ili kufanya hivyo, nywea misuli ya nyonga kana kwamba unasitisha mtiririko wa mkojo. Unaweza fanya mazoezi ili kutambua misuli fulani, kwa kusitisha mkojo katikati ya mtiririko unapokojoa. Nywea misuli hii kwa takriban sekunde kumi, mara kumi wakati mmoja, kati ya mara sita na mara kumi kwa siku.
Magoti yaniuma sana hedhi inapokaribia
Mpendwa Daktari,
Nina umri wa miaka 30 na kwa kawaida mimi hukumbwa na maumivu ya magoti unapokaribia wakati wa hedhi.
Mimi huanza kukumbwa na hisia hizi wiki mbili kabla ya hedhi kwa takriban siku tatu kisha maumivu hayo yanatoweka. Mimi hutembea sana na chakula changu huhusisha mboga kwa wingi. Uzani wangu ni kilo 53. Naomba ushauri.
Betty, Mombasa
Mpendwa Betty,
Takriban 75% ya wanawake hukumbwa na ishara kila mwezi kabla, wakati na baada ya kushuhudia hedhi. Hali hii inafahamika kama premenstrual syndrome.
Hali hii huwa na ishara mbali mbali ambazo huwa tofauti kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, na huenda zikabadilika kutoka mwezi mmoja hadi mwingine.
Dalili hizi hutoweka ukiwa mjamzito au katika kipindi cha kukatikiwa.
Huenda ishara zikawa nyepesi au kali na huenda zikahusisha ishara za kimwili, kimhemko na mabadiliko ya kitabia.
Maumivu ya viungo ni mojawapo ya ishara na ndio sababu unahisi hivyo kwenye goti lako.
Kutokana na sababu hali hii inakukumba wakati fulani wa mzunguko wa hedhi kisha kutoweka, inaashiria kwamba inasababishwa na mabadiliko ya kihomoni ya kila mwezi.
Kutembea sana na kiwango cha chini cha madini ya calcium pia huenda zinasababisha hali hii. Unapokumbwa na maumivu ya viungo, unaweza tumia barafu kutuliza sehemu hii. Pia waweza tumia dawa za kukabiliana na maumivu.