WANDERI KAMAU: Mbona Ruto ananyamazia shutuma dhidi ya Farouk Kibet?
Na WANDERI KAMAU
MNAMO Ijumaa, kulisambaa tetesi kuwa, Seneta Susan Kihika wa Nakuru amefurushwa kutoka kwa mkutano ulioandaliwa katika makazi rasmi ya Naibu Rais William Ruto, Karen, Nairobi, kwa tuhuma za kuwa “fuko” wa Chama cha Jubilee (JP).
Ilidaiwa Bi Kihika alifukuzwa kutoka mkutano huo na Msaidizi wa Kibinafsi wa Dkt Ruto, Farouk Kibet.Ingawa Bi Kihika alijitetea dhidi ya tuhuma hizo, alizitaja kuwa “propaganda zinazoendeshwa na mahasimu wake wa kisiasa.”
Katika majukwaa tofauti, si mara moja ambapo baadhi ya wanasiasa wanaomuunga mkono Dkt Ruto wamejitokeza hadharani kulalamikia kuhangaishwa na msaidizi huyo.
Mwaka jana, mbunge Aden Duale (Garissa Mjini) alirejelea “ushawishi mkubwa” wa Bw Kibet, akisema mara nyingi, ndiye mwamuzi wa mwisho kuhusu ikiwa mtu fulani atamwona Dkt Ruto au la.
Kwenye Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) wa chama cha UDA katika Uwanja wa Michezo wa Kasarani mwezi jana, Bw Kibet alionekana akigombana hadharani na Katibu Mku wa chama hicho, Bi Veronicah Maina na mwenyekiti wake, Johnson Muthama.Kama kwamba hilo halitoshi, msaidizi huyo pia amekuwa akilaumiwa na wanahabari kwa kuwatusi na kuwahangaisha kila wanapoenda katika hafla za Ruto.
Swali lililo vinywani mwa wengi ni, je Bw Kibet huwa anafanya vitendo hivyo chini ya baraka au maagizo ya Dkt Ruto? Mbona Ruto huwa ananyamazia malalamishi mengi ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi yake?
Ingawa kuna mamilioni ya Wakenya wanaomuunga mkono Dkt Ruto kuwania urais kwenye uchaguzi wa Agosti, huenda azma yake ikaanza kupakwa tope na uwepo wa “wasaidizi” kama hao katika kambi yake ya kisiasa.
Bw Kibet anaashiria mienendo hatari iliyodhihirika kutoka kwa washirika wa karibu wa marais wa awali kama Mzee Jomo Kenyatta, Daniel Moi na Mwai Kibaki, ambao walipaka tope tawala zao, licha yao kuwa maarufu na kupendwa na raia.
Katika utawala wa Mzee Kenyatta, baadhi ya washirika wake kama Mbiyu Koinange walilaumiwa sana kuwahangaisha watu waliotaka kukutana au kumwona Rais.
Marehemu Nicholas Biwott naye alitajwa kuwa miongoni mwa watu waliochangia sana Wakenya kuanza kuuchukia utawala wa Bw Moi kutokana na ukatili wake.
Uchaguzi mkuu unapokaribia, ni wakati mwafaka kwa Ruto kutoa ufafanuzi kuhusu majukumu halisi ya Farouk Kibet, la sivyo atakuwa hatarini kupoteza umaarufu kutokana na vitendo vya baadhi ya wasaidizi kama hao.
[email protected]
Next article
Nina tajriba ya kufufua uchumi, Wanjigi asema