Connect with us

General News

Mbona tusiwajaribu? – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Na BENSON MATHEKA

SIASA za urithi kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022 zinapozungumziwa, ni vigogo kama vile Raila Odinga, William Ruto, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula na Gideon Moi hutajwa.

Wanasiasa hao wameteka akili za Wakenya hivi kwamba wanasahau, nchi hii ina viongozi na wataalamu walioiva kuwa rais na kubadilisha hali ya maisha ya Wakenya.

Dkt Fred Matiang’i

Ingawa hajatangaza azima yake ya kujiunga na siasa kwenye uchaguzi mkuu ujao, Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i amekuwa akihimizwa kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Amedhihirisha kuwa mchapa kazi, mwenye msimamo asiyeyumbishwa na kelele za wanasiasa.

Kwa muda wa miaka minane ambayo amekuwa serikalini, amebadilisha na kulainisha kila wizara aliyohudumu.

Akiwa Waziri wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kati ya 2013 na 2015, alibadilisha huduma katika serikali kwa kuhakikisha kila idara inakumbatia tekinolojia. Alipanua huduma za tekinolojia katika serikali za kaunti ili kuwepo kwa uwazi na kuhamishia Kenya katika mawimbi ya utangazaji ya kidijitali. Aliendelea na ukakamavu wake katika wizara ya Elimu mnamo 2015 ambapo alikabiliana na udanganyifu katika mitihani na vyeti vikiwemo vya digrii.

Bila kuogopa, alilainisha shughuli katika Baraza la Taifa la Mitihani (KNEC) na kurejesha hadhi ya mitihani na kuimarisha viwango vya elimu, jambo ambalo lilikuwa limewashinda watangulizi wake wengi katika wizara hiyo. Alipoteuliwa kaimu waziri wa ardhi mwaka huo baada ya Bi Charity Ngilu kujiuzulu, alikabiliana na matapeli wa ardhi ambao hakuna aliyethubutu kuwagusa na kuzima mauaji katika kampuni ya mashamba ya Kihiu Mwiri kaunti ya Murang’a. Katika wizara ya usalama wa ndani anakohudumu kwa sasa, Dkt Matiang’i amekuwa kama sauti ya serikali kwa kuhakikisha utulivu nchini. Wadadisi wanasema tajiriba ambayo amepata katika wizara alizohudumu, hulka yake ya kutobembeleza na kushawishiwa na wanasiasa akiwa mwenyekiti wa kamati ya taifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Dkt Matiangi anatosha kuwa rais anayeweza kubadilisha Kenya.

“Anaweza kuleta damu mpya katika utawala Kenya. Ameiva kuwa rais,” asema mdadisi wa siasa Paul Katana.

Baadhi ya viongozi wa kaunti ya Kisii na hata mawaziri wenzake wamekuwa wakimpigia debe wakisema wako na imani naye.

Dkt Mukhisa Kituyi

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa shirika la kibiashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD) Mukhisa Kituyi ana kila kinachohitajika kuwa rais wa Kenya. Mbali na tajiriba yake pana kama mwanadiplomasia wa masuala ya kibiashara, Dkt Kituyi hana kashfa yoyote tofauti na baadhi ya wanasiasa wanaomezea mate kiti cha urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Wadadisi wanasema Dkt Kituyi hajawahi kujihusisha na siasa za ukabila ambazo zimekita mizizi nchini. Alipokuwa waziri wa biashara wakati wa serikali ya Rais Mwai Kibaki kati ya 2002 na 2007, Dkt Kituyi alishirikiana na wataalamu wengine kukuza Kenya kama kituo cha kibiashara na matokeo yake yalikuwa ni kukua kwa uchumi. Kuanzia 2008 hadi 2012, Dkt Kituyi alikuwa miongoni mwa wataalamu waliokuwa wakishauri marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu jinsi ya kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi wenye nguvu. Dkt Kituyi amepiku wanasiasa wenye majina makubwa wanaogemea siasa za migawanyiko akiwa amehudumu katika Muungano wa Afrika AU kama mshauri wa kibiashara kati ya 2011 na 2012. Kulingana na Bw Katana, Dkt Kituyi ni mmoja wa Wakenya walio na tajiriba pana ya mseto wa siasa, utawala na usimamizi na kutambuliwa kimataifa kwa sifa nzuri.

“Labda Wakenya wanapaswa kujaribu viongozi kama Dkt Kituyi ambaye haachi doa anakohudumu,” asema Katana.

Profesa Kivutha Kibwana

Kwa muda wa miaka minane na nusu ambayo amehudumu kama Gavana wa Makueni, Profesa Kivutha Kibwana amedhihirisha kwamba, viongozi wanaochaguliwa wanaweza kuwajibikia wapigakura bila tamaa. Alisimama kidete kukataa njama za madiwani kaunti yake kujitengea mamilioni badala ya kujali miradi ya kuinua maisha ya wakazi hadi wakapitisha azimio la kumtimua ofisini. Akiwa mtaalamu wa masuala ya katiba, Kibwana amedhihirisha anapenda haki na utawala wa sheria. Aliweza kujenga hospitali ya mamilioni ya pesa licha ya kupigwa vita na madiwani na Makueni ndiyo kaunti ya pekee nchini ambayo imetekeleza kikamilifu marufuku ya uzoaji wa changarawe katika juhudi za kulinda mazingira. Ili kulinda heshima yake, alivunja uhusiano wake na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akidai hajali maslahi ya raia. Kabla ya kushiriki siasa za uchaguzi mwaka wa 2003 alikuwa mtetezi wa siasa za vyama vingi na wadadisi wanasema kufikia sasa, hajawahi kuhusishwa na madai ya ufisadi.

Martha Karua

Kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua amejijenga kama mwanasiasa huru asiyeshawishiwa na mawimbi ya siasa. Ni mmoja wa viongozi wachache wanawake ambao wamewahi kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 na angali na azima ya kugombea uongozi wa nchi kwenye uchaguzi mkuu ujao. Wadadisi wanasema Karua ni mtetezi wa demokrasia na utawala bora ambaye hajiungi na mirengo ya kisiasa kufurahisha walio mamlakani.

Martha Karua sio kibaraka wa yeyote na hata kabla ya kujiunga na siasa, alikuwa akitofautiana na sera za viongozi za kukandamiza raia. Hii ndiyo ilimfanya ajiuzulu kama waziri wa haki katika serikali ya Rais Kibaki mwaka wa 2019. Ameendelea kupigania utawala bora hadi wakati huu kwa ujasiri na haogopi kukosoa viongozi hadharani.

Profesa George Magoha

Kwa muda mfupi ambao amekuwa waziri wa Elimu, Profesa George Magoha amedhihirisha kuwa na misimamo mkali asiyeyumbishwa na kelele za watu. Anatekeleza anachoamini ni halali na kinachofaa Wakenya. Akiwa daktari na mhadhiri wa miaka mingi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Magoha anatosha kuwa Rais wa nchi hii. Amethibitisha kuwa mchapa kazi asiyechoka tangu alipoteuliwa mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Mitihani la Kenya (KNEC) ambapo alianzisha mabadiliko makubwa yaliyorejesha imani katika mitihani. Kulingana na mdadisi wa siasa Geff Kamwanah, maendeleo ya dhati yanaweza kupatikana iwapo Wakenya wanaweza kuchagua wataalamu kama Magoha kuwa viongozi wao.

Salim Mvurya

Mmoja wa magavana ambao wamefanikisha maendeleo katika kaunti zao ni Salim Mvurya wa Kwale. Mtulivu na asiye na tamaa, wengi wamemtaja kama mwanamikakati shupavu anayewajibika kwa wapigakura.

Magavana wengine wanaohudumu kwa kipindi cha pili wanapohusika na siasa za mirengo kwa kujipiga kifua kujitafutia umaarufu, Bw Mvurya amekuwa akitekeleza miradi ya kuwafaa wakazi wa kaunti za Pwani iliyomfurahisha Rais Kenyatta alipozuru Kaunti ya Kwale mwaka 2020 hivi kwamba akawaambia wakazi: “Rekodi ya maendeleo ya gavana wenu ni ya kipekee. Nimefurahishwa na kazi ambayo amefanya kuhakikisha ustawi wa kaunti,” Chini ya uongozi wake kaunti ina miundomisingo bora. Ingawa hajatangaza azima ya kugombea urais, ni mmoja wa viongozi walioiva kubadilisha Kenya.

Mbona tusiwajaribu? – Taifa Leo

Martin Odour

Mtaalamu wa masuala ya uchumi Martin Odour Otieno ni mmoja wa wataalamu wa masuala ya uchumi wanaoheshimika kote ulimwenguni. Uchumi wa Kenya ulipoenda yombo 1999 wakati wa utawala wa Kanu, Rais Moi alimteua pamoja na wataalamu wengine kuufufua. Kuanzia 2007 hadi 2012, alidhihirisha kwamba usimamizi bora unaweza kujenga taasisi kwa kubadilisha Benki ya Kenya Commercial kuwa benki kubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati. Wengi wanaamini ufanisi wa sasa wa Kenya Commercial Bank ni matunda ya jasho la mwanauchumi huyo aliyeweka jiwe la msingi. Wachanganuzi wanasema kwamba, mtaalamu huyu ni mmoja wa Wakenya walioiva ambao wanaweza kuleta mageuzi ya dhati nchini wakiwa uongozini. Hata hivyo, Oduor hajawahi kueleza azima ya kugombea urais.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Trending