PAXSON Mwangi amekuwa katika sekta ya sanaa, uchoraji, kwa zaidi ya miaka mitatu.
Hata ingawa alitambua kujaaliwa kipaji cha uchoraji akiwa mdogo kiumri, alikigeuza kuwa biashara 2018.
Hatua hiyo ilikuwa baada ya kufanya mtihani wa kitaifa kidato cha nne, KCSE, ambapo anasema alichora picha ya mwanasoka tajika Cristiano Ronaldo, anayechezea klabu ya Juventus kwa sasa, anayosema ilimvutia mama yake.
Kulingana na masimulizi yake, aliichora kwa penseli.
Ilifurahisha nina yake, kiasi cha kumtaka achore picha ya babu yake. “Jaribio la kwanza halikuniridhisha, niliificha na kuchora nyingine ambayo mama aliinunua Sh200,” kijana Mwangi anadokeza.
Anasimulia kwamba pia aliichapisha mitandaoni, katika kurasa zake za Facebook na Instagram, hatua ambayo ilifungua jamvi la uchoraji-biashara.
Huku talanta yake ikiwa ya kipekee, kutokana na uchoraji kwa kutumia penseli, amekuwa akiendeshea shughuli hiyo kwenye chumba chake cha kukodi eneo la Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi.
Aidha, chumba hicho ndicho karakarana yake.
Wachoraji wengi hutumia rangi maalum aina ya acrylic, ila ubunifu wake kupitia matumizi ya penseli na kalamu ya wino, unamfanya kuwa wa kipekee.
Huduma zake kuchora zikiwa kati ya Sh1,500 – 9,500, Mwangi maarufu kama Pakii Mchoraji, anasema janga la Covid-19 limeathiri kwa kiasi kikubwa utendakazi wake.
“Kabla ya Covid, nilikuwa nikitumia majukwaa ya maonyesho ya sanaa na uchoraji kunadi umahiri wangu. Amri ya marufuku ya mikusanyiko ya umma imeathiri sekta ya sanaa kwa njia hasi,” analalamika.
Paxson Mwangi akichora picha, kwenye karakana yake eneo la Githurai. Picha/ Sammy Waweru
Huku akitumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Instagram kuhamasisha huduma zake, Mwangi anasema haijakuwa rahisi kuendesha kazi kipindi hiki taifa linang’atwa na makali ya virusi vya corona.
Mbali na Kenya, mataifa mengine ulimwenguni yanaendelea kuhangaishwa na Covid-19, ugonjwa ambao ni janga la kimataifa.
Amri ya ama kuingia au kutoka Kaunti ya Nairobi na majirani, iliyoondolewa Mei 1, 2021 na Rais Uhuru Kenyatta, ilimzuia kuzuru eneo kama vile Murang’a ambapo ana wateja kadhaa.
Kimsingi, mwanasanaa huyo analalamikia kuendelea kupuuzwa kwa sekta ya usanii na sanaa, na ambayo ina vipaji wengi.
“Kuna vijana wengi nje wamejaaliwa talanta tofauti, ila hawana majukwaa wala namna ya kuamka,” Mwangi aeleza.
Kauli yake inaoana na ya Joseph Njroroge, ambaye ni mchoraji tajika.
“Sekta ya usanii inahitaji kupigwa jeki na serikali, ina vipaji wengi sana waliojaaliwa talanta. Walichokosa ni hamasisho na fedha kujiimarisha,” Njoroge na ambaye huchorea eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, anaiambia Taifa Leo.
“Wasanii wa michoro na michongo wakiinuliwa watakuwa na mchango mkubwa katika kuangazia suala la ukosefu wa ajira, hasa miongoni mwa vijana. Changamoto zinazowakumba, ni kukosa hamasa na jukwaa la kujiimarisha. Wengi wao huishia kufa moyo,” anafafanua.
Kulingana na Njoroge, wakiimarika, ina maana kuwa serikali itakuwa imeongeza viteka vingine kukusanya kodi na ushuru.
Njoroge anasema anaendelea kupokea maombi chungu nzima ya vijana wenye nia kunoa vipaji vyao katika uchoraji.
“Ninayoshuhudia katika sanaa, ninaamini ni sawa na taswira katika ulingo wa usanii, uigizaji na gange zingine za mikono na bongo,” Njoroge asisitiza.
Kwa mujibu wa wachoraji hao, maji yamezidi unga kipindi hiki cha Covid-19.
Serikali ikiendelea kuhimiza umma kuzingatia kanuni na mikakati iliyowekwa kusaidia kuzuia msambao wa corona, wanahoji wanasanaa wangetumika kufanya hamasisho mbinu za kujikinga na pia athari za janga la Covid.
“Hiki ndicho kipindi michoro inahitajika kupasha ujumbe. Tungetumika kufanya michoro ya uvaliaji bora wa barakoa, nafasi baina ya mtu na mwenzake katika maeneo ya umma na jinsi ya kunawa mikono ili kukabili msambao wa corona,” wanasema.
Wizara ya Michezo na Turathi za Kitaifa, ndiyo yenye wajibu kuangazia masuala ya usanii na sanaa.
Ingekuwa busara ijitume kuinua sekta hiyo yenye vipaji chungu nzima, hatua ambayo itasaidia kuboresha uchumi.