[ad_1]
Sababu ni kwamba neno ‘mwenzake’ lina maana ya mtu ambaye anashirikiana na mwingine katika shughuli fulani kwa mfano biashara, masomo, siasa na kadhalika.
Linalojitokeza katika dhana hii ni ubia au ushirika ambapo hapana anayemdhibiti mwingine. Kwa upande mwingine, neno wake linaonesha kitu alicho nacho mtu kama sehemu ya mali yake au utambulisho. Maneno ‘mwenzake’ na ‘wake’ yanapotumiwa pamoja, huibua utata ambapo ni muhali kueleza iwapo kinachozungumziwa ni ushirika au umilikishi. Pili, katika neno mwenzake au mwenza, inajitokeza dhana ya umilikishi ambayo haihitaji tena kurudiwa kwa kutumia kimilikishi ‘wake’.
Katika sehemu ya pili ya mjadala huu tulieleza kuwa yamkini watumizi wa lugha ya Kiswahili huitumia dhana ‘mgombea mwenza’ na maneno yenye ukuruba wa kimaana nayo ili kuwanasibisha wanaozungumziwa (wagombea) na waliowachagua katika nafasi hizo.
Yaani, kuna ‘mgombea mwenza’ wa mheshimiwa Raila na yule wa mheshimiwa Ruto. Hata hivyo, ifahamike kuwa utata hutokea dhana ‘mgombea mwenza’ inapotumiwa kurejelea nafsi ya pili na ya tatu umoja na wingi. Sivyo ilivyo dhana yenyewe inapotumiwa kurejelea nafsi ya kwanza katika hali zote mbili.
Alhasili, ni kosa kusema ‘wagombea mwenza’ kwa maana ya watu wanaoshirikiana nao katika shughuli fulani. Maadamu dhana hiyo imeundwa kwa maneno yanayoweza kubadilika katika hali ya wingi, basi sahihi ni kusema ‘wagombea wenza’.
Kosa jingine la kisarufi linatokana na matumizi ya dhana ‘mgombea mwenza’ na wake.