Mradi wa Buxton wapata pigo tena
NA BRIAN OCHARO
MZOZO umeibuka tena kuhusu ujenzi wa nyumba za bei nafuu za Buxton, Kaunti ya Mombasa, na kutishia kukwamisha mradi huo mkubwa.
Kampuni ya Philmark System Services Ltd, imeshtaki Buxton Point Developers Ltd inayosimamia mradi huo kwa madai ya kusitisha mkataba wake kiharamu.
Kampuni ya Buxton Point inahusishwa na mfanyabiashara, Bw Suleiman Shahbal, ambaye amenuia kuwania ugavana Mombasa katika uchaguzi ujao.
Kampuni ya Philmark sasa inataka mahakama iamrishe ujenzi usitishwe hadi malalamishi yake yatakaposikilizwa na kuamuliwa.
Jaji Olga Sewe wa Mahakama Kuu ya Mombasa ameidhinisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru hati za kesi ziwasilishwe kwa pande zote husika kabla ya kesi hiyo kusikizwa.
Kampuni ya Philmark System Services Ltd imedai ilikuwa imekamilisha asilimia 70 na 40 ya awamu ya kwanza ya mradi unaohusisha sehemu A na B mtawalia.
Imedaiwa kuwa, kampuni ya Roton Construction Ltd ilikuwa imeshinda zabuni ya mradi huo lakini ilitoa kandarasi ndogo kwa Philmark System Services kukamilisha ujenzi wa sehemu A na B kwa gharama ya Sh510 milioni.
Kampuni ya Philmark System Services ilipokea barua ya kusitisha mkataba wake Februari 28.
“Licha ya kusitishwa kwa kandarasi, kampuni haijalipwa kwa kazi iliyofanywa kufikia sasa na vifaa vilivyoagizwa na kuwasilishwa katika eneo la kazi,” kampuni hiyo ikasema, kupitia kwa wakili wake, Bw Paul Magolo.
Mkurugenzi wa Philmark System Services Ltd, Bw Philemon Okello, alidai kuwa kampuni hiyo imepata hasara ya zaidi ya Sh200 milioni kufuatia hatua hiyo.
Bw Okello amedai katika hati ya kiapo kwamba washtakiwa wananuia kubomoa afisi ambayo kampuni hiyo ilikuwa ikifanyia kazi na kwamba vifaa na mashine za kampuni hiyo ambazo bado ziko katika eneo hilo, zinaharibiwa na kutumiwa vibaya.
Alitaka mahakama kutoa amri ya kubatilisha uamuzi wa Buxton Point kusitisha mkataba wake wa mradi huo, na nyingine ya kuzuia kampuni yoyote kukamilisha kazi ambayo ilikuwa imeanzishwa katika majengo hayo hadi malalamiko yake yatakaposikilizwa na kuamuliwa.
Kampuni hiyo pia inataka mahakama itoe uamuzi kwamba kusitishwa kwa kandarasi yake ilikuwa kinyume cha sheria, malipo ya kazi iliyofanywa na vifaa kuwasilishwa kwenye majengo hayo na fidia ya Sh200 milioni kutokana na hasara inayodai ilipata kwa kusitishwa kwa mkataba huo kinyume cha sheria.
Mradi huo ulianza Mei mwaka jana lakini ujenzi ulicheleweshwa kutokana na kesi nyingine iliyowasilishwa mahakamani na wapangaji waliofurushwa katika eneo hilo.
Mahakama iliporuhusu mradi huo kuanza, Kamati ya Seneti kuhusu Ujenzi pia iliagiza ujenzi usitishwe kufuatia malalamishi ya fidia, na kumwagiza Gavana wa Mombasa Hassan Joho kutoa maelezo kuhusu mradi huo.
Kando na malalamishi yaliyotolewa na baadhi ya wakazi waliohamishwa, maswali mengine ambayo huibuka ni kuhusu mkataba kati ya kampuni ya Buxton Point na Serikali ya Kaunti. Ardhi hiyo ni ya umma.
Hata hivyo, ujenzi umekuwa ukiendelea kwa kasi na awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kukamilika Mei 2022.
Mradi wa nyumba za Buxton unajumuisha ujenzi wa nyumba 600 vya chumba kimoja cha kulala, 700 vya vyumba viwili vya kulala, na 600 vya vyumba vitatu kwenye ardhi hiyo ya ekari 14.
Mradi huo ni mojawapo ya miradi mikubwa ambayo serikali ya kitaifa inatekeleza kote nchini kwa ajili ya kuongeza idadi za nyumba za bei nafuu, kwa ushirikiano na serikali za kaunti na makampuni ya kibinafsi.
Mradi huo unalenga kupunguza gharama za ujenzi wa nyumba kwani mara utakapokamilika, watu wengi watakuwa na nafasi ya kumiliki nyumba.