Connect with us

General News

Mradi wa ufugaji nyuki wasaidia jamii kujikimu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mradi wa ufugaji nyuki wasaidia jamii kujikimu – Taifa Leo

Mradi wa ufugaji nyuki wasaidia jamii kujikimu

NA SAMMY WAWERU

MUKANGU, Kijiji kilichoko Kata ya Kiine, boda ya Kaunti ya Nyeri na Kirinyaga ni tajika katika kilimo cha kahawa.

Ni katika eneo hilo Martin Mwangi na mpwa wake Samuel Muhindi, wanaendeleza ufugaji nyuki.

Waliuanza kama mradi wa kujipa pato la ziada, ila mbali na shabaha hiyo sasa unawafaa kwa kiasi kikubwa wasiojiweza katika jamii. Walizindua mradi huo wa Walker Beekeepers, 2019.

“Tulipanua mawazo yetu kufuatia ari ya wenyeji kutaka kujua zaidi kuhusu ufugaji wa nyuki ,” Mwangi asema.

Kwa wawili hao, uzalishaji wa kahawa na kufuga nyuki ni sawa na kulenga ndege wawili kwa kutumia jiwe moja.

“Kahawa huchana maua tele, na nyuki ni mdudu muhimu sana kusaidia katika uchavushaji mtambuka (cross pollination). Hivyo basi wataifaa na kugeuza chakula wanachobugia kuwa asali,” Mwangi afafanua.

Kulingana na Muhindi, waling’oa nanga kwa mtaji wa Sh50,000.

“Tulianza na mizinga 10, ambayo tuliiweka kwenye shamba la kahawa,” afichua.

Mara ya kwanza, nyuki huchukua muda wa miezi sita kuunda asali na Muhindi anadokeza walivuna jumla ya kilo 50.

Majaribio yanayofuata, huchukua wastani wa miezi mitatu, na kabla kuingilia ufugaji nyuki unashauriwa kuhusisha Mamlaka ya Uhifadhi wa Mazingira Nchini (Nema).

Miaka mitatu baadaye, wawili hao wana kila sababu ya kutabasamu kufuatia mchango wao mkuu katika jamii.

Kilele cha Walker Beekeepers kimekuwa kuzaa muungano wa Mukandima, kundi la kijamii (CBO), linalohamasisha wakazi kuhusu ufugaji nyuki na kurina asali.

“Tunawafunza haja ya kufuga nyuki, inayojumuisha kuelewa wadudu hao, kuweka mizinga shambani na jinsi ya kutunza nyuki, kuvuna asali na kusaka soko,” Mwangi aelezea.

Anaongeza: “Asali haijawahi kosa soko. Isitoshe, kiwango chetu cha uzalishaji kama taifa ni cha chini mno.”

Victor Okoth kutoka National Bee Institute, anasema Kenya huagiza nje asilimia 70 ya asali inayotumika nchini.

“Hii inaashiria kuwa tunazalisha asilimia 30 pekee. Huagiza kwa wingi kutoka Tanzania, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Sudan,” adokeza mtaalamu huyo.

Mukandima ina vituo vitatu, kimoja katika eneo la Mukangu, kingine Rumuti – Laikipia na vilevile katika Kaunti ya Baringo.

Aidha, kila kituo kina wanachama. Ada ya kusajiliwa kuwa mwanachama ni Sh200.

Kwa wasio wanachama kupata mafunzo, hutoza Sh2,000.

“Tunalenga vijana wasio na ajira, wajane na walemavu. Baada ya kupitia mafunzo, huwapa mizinga miwili na mche wa mti,” Mwangi aelezea.

“Kila mzinga unaoundwa, unahusisha miti. Tuko ange kutunza na kulinda mazingira kupitia upanzi wa miti.”

Waasisi wa mradi huo unaolenga kukabiliana na umaskini, wanakiri visa vya vijana kujitia kitanzi kwa kukosa ajira, uhalifu, matumizi ya dawa za kulevya na mihadarati na vita vya kijinsia (GBV), vimepungua kwa kiasi kikubwa eneo la Mukangu.

Walker Beekeepers pia hutengeneza mizinga katika karakana yake, mmoja ikiuza Sh4,500.

“Shughuli zingine, ni kutengeneza sabuni, mishumaa na mafuta kwa kutumia nta ya nyuki,” Muhindi asema.

Licha ya wawili hao kujituma kunusuru jamii, safari yao haijakuwa rahisi.

Ukosefu wa fedha za kutosha, kutoa mafunzo na msaada wa mizinga ni mojawapo ya changamoto, wakiisihi serikali kuu na kaunti kuwapiga jeki.