Connect with us

General News

Msimamizi mpya wa Mumias Sugar apaswa kuungwa mkono kikamilifu – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Msimamizi mpya wa Mumias Sugar apaswa kuungwa mkono kikamilifu – Taifa Leo

CHARLES WASONGA: Msimamizi mpya wa Mumias Sugar apaswa kuungwa mkono kikamilifu

Na CHARLES WASONGA

NI habari njema kwa wakulima wa miwa katika eneo la Mumias na wakazi wa kaunti ya Kakamega kwa ujumla baada ya kampuni ya Sukari ya Mumias kuwekwa chini ya msimamizi mpya.

Mnamo Desemba 22, 2021 meneja mrasimu aliyeteuliwa na Benki ya Kenya Commercial (KCB) kuendesha shughuli za kampuni hiyo, Ponangipali Rao, alipokeza usimamizi wake kwa kampuni ya Sarrai Group kutoka Uganda.

Kulingana na mkataba wa ukodishaji uliotiwa saini na Bw Rao na mwakilishi wa mwekezaji huyo mpya Sarbi Rai, kampuni ya Sarrai itaendesha shughuli za kitengo cha utengenezaji sukari katika kampuni ya Mumias kwa kipindi cha miaka 20.

Zamani, kampuni ya Mumias ilikuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 250,000 kwa mwaka lakini ikaporomoka kutokana na usimamizi mbaya, ufisadi, mzigo wa madeni na kuharibika kwa mitambo ya kusaga miwa.

Juhudi za serikali kuu za kuifufua kwa kuipa jumla ya Sh3 bilioni kuanzia 2013 hadi 2017 hazikuzaa matunda.

Ndio maana mnamo 2019 kampuni hiyo iliwekwa chini ya usimamizi wa mrasimu ili kulinda mali yake isinadiwe kulipia deni la zaidi ya Sh11 bilioni.

Kampuni ya Sarrai sasa imetwikwa wajibu mkubwa wa kufufua kampuni hii ya sukari ya Mumias ambayo kusambaratika kwake kuliwaacha maelfu ya wakazi bila kitega uchumi huku biashara ambazo ziliitegemea pia zikiporomoka.

Nao wakulima wa miwa katika eneo Magharibi ambao kwa miaka mingi waliwasilisha miwa yao katika kampuni hii waliachwa bila chanzo cha mapato hali iliyochangia wengi wao kuacha kilimo cha miwa na kukumbatia kilimo cha mazao mengine.

Kuwekwa kwa kampuni hii chini ya usimamizi mpya sasa kutawapa shime ya kurejelea kilimo cha miwa kwa matumaini kuwa watafaidi kama zamani.

Lakini ili wakulima na wakazi kufaidi kikamilifu, kampuni ya Sirrai inahitaji mazingira bora na faafu ya kuendeshea shughuli zake.

Inahitaji uungwaji mkono kutoka kwa serikali kuu na serikali ya kaunti ya Kakamega, viongozi wa kisiasa wakulima na wenye hisa katika kampuni hii ya Mumias.

Vile vile, kampuni hii ya Uganda iungwe mkono na kampuni zingine ambazo zilishindania usimamizi wa kampuni lakini zikabwagwa na Sarrai Group.

Kampuni hizo ni kama vile West Kenya Sugar, Devki Group, Kibos Sugar, miongoni mwa nyingine.

Hatua ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kama vile Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na wabunge Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) na Peter Nabulindo (Matungu) kuchangamkia ujio wa usimamizi mpya wa kampuni hiyo ya sukari ni nzuri.

Hii ina maana kuwa viongozi hawa hawataingilia shughuli za mwekezaji huyo mpya, hali ambayo itakuwa na manufaa makubwa kwa wakulima na wenye hisa wa kampuni hii.

Sasa ni wajibu wa wanasiasa hawa kuwahimiza wakulima kukuza miwa kwa wingi ili kampuni hii isikabiliwe na uhaba wa malighafi ya kuendeshea shughuli zao.

Kwa upande, wake kampuni ya Sarrai Group iendeshe shughuli zake kwa kuzingatia sheria zinazoongoza sekta ya miwa nchini na ambazo zinatekelezwa kwa usimamizi wa wizara ya kilimo.

Kwa mfano, kampuni hii ifuate kanuni iliyochapishwa na Waziri wa Kilimo Peter Munya mwaka 2020 na inayohitaji kwamba wakulima walipwe wiki moja baada ya kuwasilisha miwa yao kwa kampuni za sukari.

Hii itaongeza ari ya wakulima wa miwa ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiteseka baada ya malipo yao kucheleweshwa.