Connect with us

General News

Mtihani wa KCPE kuanza rasmi leo – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mtihani wa KCPE kuanza rasmi leo – Taifa Leo

Mtihani wa KCPE kuanza rasmi leo

NA DAVID MUCHUNGUH

ZAIDI ya watahiniwa 1.2 milioni wataanza rasmi leo Jumatatu Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) katika vituo 28,316 kote nchini.

Watahiniwa watafanya mtihani huo kwa siku tatu zijazo baada ya kusoma kwa ratiba iliyoonekana kukimbizwa.

Hili ni baada ya janga la virusi vya corona kuvuruga mpangilio wa masomo nchini tangu mwaka 2020.

Watahiniwa hao walifanya majaribio ya mtihani huo Ijumaa wiki iliyopita.

Leo Jumatatu, watafanya mitihani ya Hisabati, Kiingereza na Insha.

Ijapokuwa mtihani wa mwaka huu utafanyika huku kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti zikiendelea, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, amepiga marufuku mikutano ya kisiasa katika shule zinazotumika kama vituo vya mitihani.

Idadi ya watahiniwa mwaka huu ni 33,755 zaidi ikilinganishwa na wale waliofanya mtihani wa mwaka 2020.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Dkt David Njeng’ere, aliiambia Taifa Leo kwamba matayarisho yote yamekamilika.

Alisema wakurugenzi wote wa elimu katika kaunti na wenzao katika Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC) wamewaarifu wasimamizi wa vituo na wale wa mitihani kuhusu majukumu watakayotekeleza.

Mitihani hiyo imewekwa kwenye vituo 491 vya kontena ambavyo vinalindwa kwa muda wa saa 24 na walinzi waliojihami vikali.

Kufuli za kontena hizo zimewekwa na wakurugenzi wa elimu wa kaunti ndogo na manaibu wa kamishna wa kaunti.

Wamepangiwa kufungua kontena hizo saa 12.30 alfajiri na kuanza usambazaji wa vifaa vya mitihani.

“Vifaa vya mitihani vinafaa kukabidhiwa wasimamizi wa vituo wakiwa wameandamana na maafisa wa usalama waliojihami,” akasema Dkt Njeng’ere.

Alisema kuwa hali ya barabara imeimarika sana nchini, hatua inayotarajiwa kurahisisha usafirishaji wa vifaa hivyo.

KNEC imebuni kituo maalum ambacho kitatumiwa kurahisisha mawasiliano na mchakato wa kusimamia mtihani huo kote nchini.

Prof Magoha alisema kuwa shule ambazo ziko mbali kutoka kwa vituo vya kuhifadhia mitihani ndizo zitapokea mitihani hiyo kwanza huku zilizo karibu zikiwa za mwisho kupokea.

“Mtihani huo uko salama. Tumedhibiti kila hali. Ijapokuwa makundi ya watu ambao wamekuwa wakisambaza mitihani ghushi bado yapo, hayajafanikiwa kupata chochote. Watahiniwa wasikubali kupotoshwa,” akasema waziri, alipohutubu katika Shule ya Upili ya Senior Chief Koinange, Kaunti ya Kiambu wikendi.

Alitoa hakikisho kwamba kutakuwa na helikopta za kutosha kupeleka mitihani katika maeneo yanayokumbwa na changamoto za kiusalama.

Baadhi ya maeneo hayo ni Kaunti ya Baringo, ambako watu saba waliuawa Jumamosi usiku, eneo la Isiolo Kaskazini ambako watu 11 wameuawa kwa muda wa siku mbili kati ya maeneo mengine.

[ad_2]

Source link

Comments

comments

Facebook

Trending