KINARA wa ANC Musalia Mudavadi angefaa kuwania wadhifa wa uongozi katika uchaguzi mkuu ujao kama mbinu ya kujifufua kisiasa hata Kenya Kwanza ikipoteza uchaguzi mkuu ujao.
Bw Mudavadi angemuiga kinara mwenzake Moses Wetang’ula na kuwania Useneta au Ugavana.
Hii ni kwa sababu huenda akajipata katika kijibaridi cha kisiasa kwa miaka mingine mitano iwapo Muungano wa Kenya Kwanza hautashinda uchaguzi ujao.
Bw Wetang’ula ambaye pia ni kinara wa Ford Kenya amechukua tahadhari na sasa atatetea kiti chake cha Useneta Bungoma.
Muda wa wawaniaji wa viti mbalimbali kando na Urais kuwasilisha stakabadhi zao ulikamilika Jumatatu na Bw Mudavadi hakuwa miongoni mwao.
Bw Wetang’ula ameahidiwa wadhifa wa Uspika katika Bunge la Kitaifa iwapo Kenya Kwanza itatwaa uongozi wa nchi.
Hata hivyo, lazima pamoja na Bw Mudavadi ambaye ameahidiwa cheo cha waziri mwenye mamlaka makubwa, masharti ni kuwa lazima wahakikshe Dkt Ruto anazoa asilimia 70 au zaidi za kura katika jamii ya Mulembe.
Kuna uwezekano kuwa hata iwapo Naibu Rais Dkt William Ruto atashinda urais na viongozi hao walemewe kuhakikisha anapata asilimia 70 au zaidi, huenda bado wakokosa nyadhifa hizo.
Je, Mudavadi atapata hifadhi wapi?
Mwanzo hilo sharti la asilimia 70 ni gumu ikizingatiwa jamii ya Waluhya kwa asilimia kubwa wamekuwa wakimpigia kiongozi wa ODM Raila Odinga kura katika chaguzi tatu zilizopita.
Isitoshe, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu Bw Odinga ambaye anawania Urais kwa tikiti ya Azimio la Umoja naye ametoa ahadi tele kwa Waluhya akichukua uongozi wa nchi.
Tayari ametenga nyadhifa za uspika, Waziri wa Fedha na Ulinzi kwa mbunge wa zamani wa Emuhaya Kenneth Marende, Gavana Wycliffe Oparanya, na Eugene Wamalwa mtawalia.
Ukiingatia mkondo wa kisiasa Magharibi, Bw Mudavadi angemeza mate machungu na kuwania useneta, ugavana au hata ubunge wa Sabatia kama njia ya kujinusuru matarajio yake ndani ya Kenya Kwanza yasipotimia.
Katika siasa huko si kujidunisha kwa sababu akishikilia moja kati ya nyadhifa hizo uwepo wake au mtikiso wake utahisiwa na bado atakuwa na uwezo wa kudumisha nafasi yake kama mwanasiasa aliye na ushawishi katika siasa za Mulembe.
Bw Mudavadi amekuwa nje ya serikali kwa miaka 10 tangu 2013. Kabla ya uchaguzi wa 2007, pia alikuwa hashikili wadhifa wowote baada ya kulambishwa sakafu na Moses Akaranga katika uchaguzi wa 2002.
Iwapo Kenya Kwanza italemewa Agosti 9 hilo litamaanisha baridi nyingine ya miaka mitano kwa Bw Mudavadi.
Bila shaka hili litaathiri siasa zake ikizingatiwa kuwa kuna vigogo wengine wa kisiasa wanaochipuka Magharibi ambao watachukua nafasi yake.? Kuna dhana kutokana na unabii wa marehemu Elijah Masinde kuwa uongozi utaingia Magharibi kupitia Ziwa Viktoria.
Iwapo Bw Odinga atatwaa Urais, basi kuna dhana kuwa atampendekeza mwanasiasa kutoka Magharibi kumrithi.
Ingawa siasa hubadilika, itakuwa vigumu kwa Bw Odinga kumtaja Bw Mudavadi kama mrithi wake ilhali hajamuunga mkono na vilevile pia ana wandani wapya ambao wamemsaidia kujivumisha Magharibi.
Kwa muda wa miaka mitano iliyopita, Bw Mudavadi aliwapa wafuasi wake wengi matumaini kuwa angefika debeni mara hii.
Hata hivyo, wengi walitamaushwa na hatua yake ya kumuunga Dkt Ruto na pia kukosa wadhifa wa mwaniaji mwenza.
Angefanikiwa kuwania wadhifa wa ubunge, useneta au ugavana kisha ashinde naye Dkt Ruto pia ashinde bado angekuwa pazuri kwa sababu bado angekuwa na nafasi ya kujiuzulu na kuchukua ule wa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka makubwa.