Connect with us

General News

Mwanahabari Eliud Waithaka azikwa Nyandarua – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mwanahabari Eliud Waithaka azikwa Nyandarua – Taifa Leo

Mwanahabari Eliud Waithaka azikwa Nyandarua

NA MWANGI MUIRURI

MWANDISHI wa habari Eliud Kimotho Waithaka wa Kaunti ya Laikipia aliyeaga dunia Ijumaa wiki jana hatimaye amezikwa leo Alhamisi nyumbani kwao katika Kaunti ya Nyandarua.

Majonzi yalitanda katika kijiji cha Ramuga-Sabuga kilichoko viungani mwa mji wa Dundori Gwa Kiongo huku waombolezaji wakimmiminia mwendazake sifa kedekede.

Bw Waithaka aliyezaliwa mwaka wa 1979 ameacha wajane wawili na watoto wanne – wawili wa kiume.

Jamaa na marafiki wampa mwanahabari Eliud Waithaka heshima za mwisho. PICHA | MWANGI MUIRURI

Miongoni mwa wanasiasa waliomwomboleza kama aliyekuwa mwadilifu kazini ni Gavana wa Laikipia Bw Ndiritu Muriithi, aliyekuwa mwenyekiti wa Mungiki Bw Maina Njenga, Mbunge wa Kieni Bw Kanini Kega, wabunge Ali Deddy wa Laikipia Mashariki, Patrick Mariru wa Laikipia Magharibi na Sara Korere wa Laikipia Kaskazini. Wengine ni Seneta John Kinyua pamoja na madiwani wa Kaunti hiyo.

Waandishi wa habari walishirikiana na wadau walioleta pamoja rafiki wake wengi mitaani, wafanyabiashara na mashirika kuandaa mazishi hayo ambayo bajeti yake ilikuwa Sh0.5 milioni.

Marehemu aliaga dunia baada ya kutatizwa na mwili kwa muda mfupi na ambapo aliaga akipelekwa hospitalini na waandishi wenzake.

Hadi kifo chake, alikuwa amehudumu kama mwalimu, fundi wa magari, mwana kwaya katika imani ya Kikatoliki na hatimaye akajiunga na uandishi habari mwaka wa 2005.

Alianza akiwa mwandishi wa kampuni ya Royal Media Services (RMS) akiwajibikia redio ya Inooro FM Kaunti ya Laikipia.

Baadaye alihamia gazeti la The Star ambalo alikuwa akiwajibikia akiwa mjini Nanyuki hadi kifo chake.

Alikuwa akijihusisha na habari kuhusu usalama, siasa na makala ya kijamii katika Kaunti za Laikipia na Samburu.

Kama aliyekuwa ameathirika na ghasia za kikabila katika Kaunti ya Narok mwaka wa 1992, kiasi kwamba familia yao ilifurushwa na ikahamia Nyandarua, Bw Waithaka alikuwa akijituma kwa kujitolea kuangazia maovu ya misukosuko katika jamii.

“Ninyime kila kitu lakini uniachie uhai wangu ndani ya amani,” Bw Waithaka alikuwa akisisitiza.

Kifo chake

Aidha, alikuwa akiangazia masuala ya watoto mayatima.

Bw Waithaka alikuwa akitatizwa na afya kwa muda na taarifa kutoka kwa familia na marafiki zilisema kwamba alikumbwa na hitilafu ya kufungana pua.

“Mimi nilipigiwa simu asubuhi na rafiki yetu mwingine akiniarifu kuwa nikimbie haraka iwezekanavyo hadi nyumbani kwa Bw Waithaka kwa kuwa alikuwa amelemewa kiafya,” akasema Bw James Murimi ambaye ni mwandishi wa Nation Media Group katika Kaunti ya Laikipia.

Bw Murimi anasema kuwa waliabiri gari kwa dharura akiwa na waandishi wengine na kufika katika Nyumba ya Bw Waithaka.

“Tulibisha mlango na akatuamkua akiwa ndani. Hakuwa amefunga mlango na ajabu ni kwamba, kufika kwa kitanda chake ambako alikuwa amelala, alikuwa haongei tena,” Bw Murimi akasema.

Aliongeza kuwa walimpeleka hadi hospitali kuu ya Nanyuki ambapo wahudumu waliompokea walimtangaza kuwa maiti.

“Tuko katika hali ya mshangao na hatuamini kuwa ukarimu, ucheshi, uungwana na mkweli wa urafiki ametuacha. Tulilia kuona akiandaliwa kuwekea katika jokovu ya mochari ya Nanyuki,” akasema Bw Murimi.