Connect with us

General News

Mzee Kibaki aunganisha Azimio, UDA – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Mzee Kibaki aunganisha Azimio, UDA – Taifa Leo

Mzee Kibaki aunganisha Azimio, UDA

NA LEONARD ONYANGO

WANASIASA wa mirengo ya Azimio na Kenya Kwanza jana walizika tofauti zao za kisiasa wakati wa hafla ya kutoa heshima kwa mwili wa Rais wa Tatu wa Kenya Mwai Kibaki katika majengo ya Bunge.

Wandani wa Naibu wa Rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga ambao wanashindana kwenye kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Jumatatu walikuwa wakipigana pambaja – tofauti na hapo awali ambapo wamekuwa wakirushiana cheche za maneno katika mikutano ya kisiasa.

Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alionekana akizungumza na Dkt Ruto na hata kukumbatiana kwa tabasamu.

Bw Musyoka pamoja na kinara wa Kanu Gideon Moi Januari 2022, walitoroka mkutano wa kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, baada ya kupashwa habari kwamba Naibu wa Rais Ruto alikuwa akielekea katika ukumbi wa Bomas ambapo kulikuwa na hafla.

Ni siku hiyo ambapo Bw Mudavadi alitangaza rasmi kuunga mkono Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais.Kambi ya Naibu wa Rais pia imekuwa ikidai kwamba Bw Musyoka amenyakua ardhi katika eneo la Yatta Machakos – madai ambayo yalilazimu kiongozi wa Wiper Agosti 2021 kwenda katika makao makuu ya Idara ya Uchunguzi (DCI) ambapo alijiondolea lawama.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya – ambaye ni mwandani wa Rais Uhuru Kenyatta – aliandamana na Dkt Ruto katika chumba cha kutoa rambirambi kwa familia ya Kibaki ambapo walipokelewa na mwanawe Jimmy Kibaki.

Jimmy tayari ametangaza kuunga mkono mwniaji wa urais “nitakayeonyeshwa na Rais Kenyatta”.

Gavana wa Kitui Charity Ngilu ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Baraza Kuu la Azimio na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula pia walikuwa na mazungumzo ya muda mrefu katika majengo ya Bunge kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kuwasili.

Bw Odinga pia amekatiza ziara yake nchini Amerika na atarejea humu nchini kesho badala ya Jumamosi ili kuhudhuria hafla ya kitaifa ya kumuaga Hayati Kibaki Ijumaa uwanjani Nyayo, Nairobi, kabla ya mwili kusafirisha hadi Othaya, Kaunti ya Nyeri, kwa ajili ya mazishi.

“Mwaniaji wa urais wa Azimio Raila Odinga amefupisha ziara yake nchini Amerika na atarejea Jumatano kwa ajili ya hafla ya kitaifa ya mazishi ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki,” akasema Prof Makau Mutua, Msemaji wa Sekretariati ya Kampeni za Azimio.

Siasa, hata hivyo, ilijitokeza baada ya Rais Kenyatta kuonekana kutokumchangamkia naibu wake Dkt Ruto na hata kukosa kumsalimia kwa mkono alipowasili katika majengo ya Bunge.

Hatua ya Rais Kenyatta kukwepa kusalimia Dkt Ruto kwa mkono ilionekana kukera wandani Naibu wa Rais wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na Seneta Maalumu Millicent Omanga.

“Mbona hakuvalia glovu ili awasalimie viongozi wenzake badala ya kuwakwepa?” akauliza Bw Murkomen.

Naye Bi Omanga alifoka: “Inamaana kwamba siku hizi Rais hasalimii kwa mkono viongozi wenzake?”

Rais Kenyatta amegeuka hasimu wa kisiasa wa Dkt Ruto na kiongozi wa nchi ambaye anaunga mkono Bw Odinga, amekuwa akishutumu mrengo wa Naibu wa Rais kwa “kunitusi na familia yangu”.

Tofauti ya kisiasa ilijitokeza baina ya mbunge Maalumu Maina Kamanda wa Azimio na mwenzake wa Kiharu Ndindi Nyoro wa Kenya Kwanza ambapo wawili hao walirushiana cheche za maneno kwa dakika kadhaa katika majengo ya Bunge.

Bw Kamanda alikataa kumsalimia kwa mkono Bw Nyoro hivyo wabunge waliokuwa karibu wakajaribu kuwapatanisha.

Jumatatu, wananchi waliruhusiwa kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Rais Mstaafu Kibaki tofauti na ratiba ya awali iliyoonyesha kuwa umma ungeanza kutazama mwili huo kati ya leo Jumanne na kesho Jumatano.

Wanasiasa wa mmungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto pia walitumia hafla ya Jumatatu kudai uchaguzi huru na haki.

“Tunachotaka ni uchaguzi huru na wa haki. Vyombo vya dola visitumiwe kuiba kura. Hata Kibaki angekuwa hai hangependa kuona kura zikiibwa,” akasema Bw Mudavadi.