WANDERI KAMAU: Askofu Anthony Muheria: Nahodha ‘atakayelifufua’ upya Kanisa nchini
NA WANDERI KAMAU
WAKATI ghasia za uchaguzi tata wa mwaka 2007 zilipotokea, moja ya taasisi zilizolaumiwa pakubwa kwa kutotekeleza majukumu yake ifaavyo ni kanisa.
Viongozi wa makanisa na mashirika mengine ya kidini walijipata kwenye lawama kubwa—wakikosolewa vikali kwa kutazama tu, mapigano yakiendelea katika sehemu tofauti nchini bila kutoa sauti yoyote.
Bila shaka, misimamo na dhana za watu wengi kuhusu umuhimu na mchango wa mashirika ya kidini kwenye ujenzi wa taifa zilibadilika.
Wengi waliyaona makanisa kama taasisi zisizokuwa na ushawishi wowote kwenye mwelekeo wa nchi, huku baadhi ya viongozi wakilaumiwa kwa kuwa vibaraka wa serikali zilizopo.
Hilo ni bila kujali ikiwa sera inazotekeleza zinawafaa raia au la.
Hata hivyo, huenda kanisa limeanza kujinasua kutoka kwa mtazamo huo kutokana na uongozi mzuri unaodhihirishwa na baadhi ya viongozi.
Baadhi ya viongozi hao ni Askofu Anthony Muheria wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Nyeri.
Kihistoria, Nyeri ni miongoni mwa vitovu vikuu vya imani ya Kikatoliki nchini.
Eneo hilo ni miongoni mwa maeneo ya mwanzo ambako Wamishenari kutoka Italia walikita kambi, mara tu baada ya kuwasili nchini mwishoni mwa karne ya 19.
Je, yawezekana Askofu Muheria anawakilisha mbegu ya kiimani iliyopandwa na Wamishenari hao?
Ijapokuwa askofu huyo amekuwa akisifiwa katika majukwaa tofauti kutokana na uungwana na weledi wake mkubwa katika masuala ya kiimani na uongozi, hilo lilidhihirika pakubwa wakati wa mazishi ya kitaifa ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki.
Ni wazi Askofu Muheria ni kiongozi mwenye upekee mkubwa.
Dhihirisho la kwanza la uungwana wa kipekee ni jinsi alivyodhibiti ratiba ya kuendesha mazishi hayo—hasa hotuba zilizotolewa na wanasiasa.
Kinyume na mazishi mengine, Askofu Muheria alimkumbusha kila mwanasiasa aliyepewa nafasi kumwomboleza Mzee Kibaki kwamba ombi la familia yake ni kusiwepo na matamshi yoyote ya kisiasa.
Hilo lilidhihirika wazi kwenye mazishi ya kitaifa katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo, Nairobi, na nyumbani kwake katika eneo la Othaya, Kaunti ya Nyeri.
Kitendo cha pili ni jinsi alivyomdhibiti barobaro Allan Makana, aliyefika katika jukwaa Uwanja wa Nyayo, akitaka kupewa nafasi kuwahutubia waombolezaji “kwa dakika mbili tu.”
Kwa wengi, hilo lilikuwa tukio la kushangaza, ambapo kwa kawaida, alitarajiwa kuviagiza vikosi vya usalama kumkabili vikali kwa kukiuka itifaki.Hata hivyo, aliwarai kutomdhulumu, akimtaja kuwa “Mkenya aliyezidiwa na hisia” kutokana na kifo cha Mzee Kibaki.
Ijapokuwa kifo cha Mzee Kibaki ni pigo kubwa kwa familia yake na nchi nzima kwa jumla, kilitoa nafasi kwa kanisa kujinasua upya na kurejesha tena usemi na ushawishi wake nchini. Mwamko huo nduo tunaomba uwepo tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti.
Heko Askofu Muheria! Wewe ndiye ‘Joshua’ anayetazamwa kufufua tena usemi wa kanisa kama ilivyokuwa katika miaka ya tisini.
[email protected]
Next article
Wawaniaji huru wa urais ni vibaraka wa serikali –…