Ni vigumu kumwomboleza mwanasiasa Kibaki bila tamko la kisiasa – Raila
NA SAMMY WAWERU
KAULI za kisiasa zilipigwa marufuku katika ibada ya kumuaga Rais mstaafu Mwai Kibaki, iliyofanyika katika uwanja wa Nyayo, Nairobi, Ijumaa, Aprili 29, 2022.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Katoliki, Jimbo la Nyeri, Bw Antony Muheria alisema uamuzi huo ulitokana na pendekezo la familia hafla hiyo kutogeuzwa ukumbi wa siasa.
Askofu Muheria pia alisema amri hiyo ilienda sambamba na sheria za Kanisa la Katoliki, lililopiga marufuku siasa kwenye makanisa yake.
“Familia imeomba ibada ya wafu ya Mzee Kibaki isiwe jukwaa la siasa,” akasema Bw Muheria.
Rais Kibaki alikuwa muumini wa Katoliki, na baada ya kanisa kukamilisha ratiba yake, Askofu Muheria alisema viongozi wachache pekee ndio watapewa fursa kutoa risala za pole.
“Kila msemaji azungumze dakika nne pekee,” akasema.
Hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii, mwanawe, Jimmy Kibaki, kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu wa Rais William Ruto, ndio walikuwa wamehutubia waombolezaji.
Bw Odinga hata hivyo alikosoa msimamo wa familia ya mwendazake na kanisa, akidai isingewezekana kukosa kumuomboleza kiongozi aliyekuwa mwanasiasa bila kushirikisha siasa.
“Sijui tutakavyoweza kumuomboleza mwanasiasa bila kuzungumza siasa,” Waziri Mkuu huyo wa zamani akaelezea.
Bw Raila alihudumu kama Waziri Mkuu, chini ya serikali ya mseto iliyoongozwa na Rais Kibaki.
Aidha, Mzee Kibaki aliongoza Kenya kati ya 2003 hadi 2013.
“Nimempoteza kiongozi aliyekuwa akinishauri,” Raila akasema, akisimulia ushirikiano wake na Mzee Kibaki.
Vilevile, alirejelea mapatano kati yake na Rais huyo mstaafu, baada ya machafuko ya uchaguzi mkuu 2007.
Mzee Kibaki alifariki Ijumaa wiki jana akiwa na umri wa miaka 90.
Atazikwa nyumbani kwake Othaya, Kaunti ya Nyeri kesho Jumamosi, Aprili 30, 2022.
Next article
Ashuu ashusha pumzi kwa muda