Connect with us

General News

Nitakuwa na mshauri maalum wa masuala ya wanawake, Nassir asema – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Nitakuwa na mshauri maalum wa masuala ya wanawake, Nassir asema – Taifa Leo

Nitakuwa na mshauri maalum wa masuala ya wanawake, Nassir asema

NA FARHIYA HUSSEIN

WANAWAKE katika Kaunti ya Mombasa watapata nafasi ya mshauri maalum wa gavana kuhusu maswala yao, mwaniaji wa kiti cha ugavana Abdulswamad Nassir amesema.

Bw Nassir anawania kumrithi Hassan Joho kupitia tiketi ya Orange Democratic Movement (ODM) katika uchaguzi wa Agosti 9.Alibainisha lengo la kubuni nafasi hiyo ni kumshauri gavana kuhusiana na masuala ya wanawake.

Akizungumza katika eneo la Changamwe Bw Nassir alisema: “Ikiwa unataka kuboresha jamii basi unapaswa kufanya hivyo kupitia wanawake. Wao ndio wanaoipeleka jamii mbele.”

Pia aliwaahidi wanawake theluthi moja ya serikali yake inavyotakikana kisheria.

Bw Nassir ambaye pia ni mbunge wa Mvita alisema ni lengo endelevu kwani amewateua wanawake kuongoza sekta muhimu katika kipindi chake cha ubunge.

“Wanawake wanafanya mambo ya ajabu. Nina wanawake wanaoshikilia nyadhifa za CDF katika Mvita. Mwenyekiti wa huduma za jamii ni mwanamke pamoja na ile ya Uwezo Fund. Na wanafanya mambo makubwa,” alisema Bw Nassir.

Aliongezea pia ataanzisha mpango maalum wa akina mama waliozaa na waume zao kuwaacha au kufariki.

“Kutakuwa na mpango maalum utakaoundwa kwa ajili ya akina mama hao. Tunapaswa kuwaunga mkono wanawake wetu. Mpango huo utajumuisha pia wale waliopata mimba za mapema. Hakuna mwanamke atakayeachwa nyuma katika serikali ijayo ya kaunti,” akasema Bw Nassir.

Wakati huo huo, wakazi wa Mombasa wamekaribisha uamuzi huo na kumuomba Bw Nassir kuzingatia kumteua naibu gavana wa kike.

“Tunathamini na kuelewa fikira za Bw Nassir. Lakini itakuwa muhimu zaidi ikiwa atachagua mwanamke kama mgombea mwenza wake. Ni wakati wanawake wajihisi kuwa sehemu ya serikali ijayo ya kaunti,” alisema Halima Abdulaziz.

Bi Christine Titus, mkazi mwingine, alisema wanawake zaidi wanapaswa kujumuishwa katika kazi za uwaziri wa kaunti.