Nitaongoza Wakenya kupata uhuru wa kiuchumi – Raila
NA SAMMY WAWERU
KIONGOZI wa Narc-Kenya, Martha Karua alikuwa na wakati mgumu kutuliza umati uliojitokeza kumsikiliza kinara wa ODM, Raila Odinga eneo la Kutus, Kirinyaga.
Raila alizuru eneo hilo Jumatatu, kutafuta uungwaji mkono katika uchaguzi mkuu Agosti 9, 2022 akilenga kumrithi Rais Uhuru Kenyatta.
Ilichukua muda Bi Karua kutuliza umati uliomzomea.
“Sisi hatutaki watu wa kuharibia wengine mikutano yao. Ninawaomba mheshimu baba (akimaanisha Raila Odinga). Waliolipwa kuja kuharibu mkutano wa baba, hatutakubali. Waandae mikutano yao hatutaihudhuria,” Karua akasema, akiwataka maafisa wa polisi kusaidia kutuliza waliotaka kuzua fujo.
Licha ya mtafaruku huo wa Kutus, Raila alihutubia waliojitokeza wakimshangilia alivyouza sera zake.
“Mwaka huu ni wa ukombozi wa tatu. Ukombozi wa kwanza ulikuwa wa uhuru, wa pili Katiba, na wa tatu ni wa kiuchumi,” Waziri Mkuu huyo wa zamani akaelezea.
Vilevile, alisisitiza lengo lake ni kupambana na maadui watatu: Ugonjwa, ujinga na maskini.
Chini ya muungano wa Azimio, Bw Raila pia alikuwa ameandamana na gavana wa Laikipia, Nderitu Muriithi, mbunge mwakilishi wa wanawake Murang’a, Sabina Chege, naibu gavana Nyeri, Caroline Karugu, miongoni mwa viongozi na wanasiasa wengine wanaompigia debe.
“Ukiona mtu analeta fujo kwenye mkutano wa mtu mwingine, hana sera wala ajenda,” Bw Muriithi akasema, akikashifu waliozomea Karua.
Jumatatu, ilikuwa siku ya pili Bw Raila kutafuta uungwaji mkono Mlima Kenya, Jumapili akikita kambi Nyeri.
Mnamo Jumamosi, aliungana na Rais Kenyatta katika mazishi ya Rais wa tatu wa Kenya, Mzee Mwai Kibaki aliyezikwa nyumbani kwake Othaya, Nyeri.
Naibu Rais Dkt William Ruto ambaye pia anasaka kura kuingia Ikulu, amekuwa akidai eneo la Kati ni ngome yake ambako anasema ana ufuasi mkubwa Mlima Kenya.