NLC yazuiwa kununua ardhi hewa ya Sh668m
NA BRIAN OCHARO
MAHAKAMA ya Mazingira na Ardhi mjini Mombasa imeagiza Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) isilipe kampuni moja fidia ya Sh667.9 milioni kwa ardhi inayodaiwa haipo.
Kulingana na hati zilizowasilishwa kortini, NLC inadaiwa ilitaka kulipa kampuni ya Dopp Investment Ltd pesa hizo kwa kutegemea hatimiliki bandia wakati wa ujenzi wa reli ya SGR.
Makampuni ya Kahia Transporters na Trade Lead Ltd yalipinga utoaji wa fidia hiyo.
Kampuni ya Dopp Investment Ltd ilikuwa imeomba mahakama iamuru kuachiliwa kwa pesa hizo, ambazo inadai ziliidhinishwa na NLC baada ya ardhi yake yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 13.8 kuchukuliwa na Shirika la Reli la Kenya (KRC).
Hata hivyo, makampuni hayo mawili yameteta kuwa ardhi ambayo NLC inadai ilipimwa na kusajiliwa mwaka wa 1991 haipo na kwamba hati zinazotolewa kwake si za kweli.
Jaji Nelly Matheka anayeshughulikia kesi hiyo alikataa ombi la kuamuru pesa hizo ziachiliwe mara moja kwa kampuni ya Dopp Investment Ltd, akibainisha kuwa madai mazito ya kutokuwepo kwa ardhi na stakabadhi bandia lazima yabainishwe kwanza.
“Haya yote ni maswala yanayohitaji kusikilizwa. Masuala haya yanahitaji kusikilizwa kikamilifu kwa hivyo amri ya kufanya malipo hayo hayawezi kutolewa,” alisema jaji huyo.
KRC na NLC zimeorodheshwa kama washtakiwa katika kesi hii huku Kahia Transporters, Trader Lead Ltd, na watu wengine wanne kama wahusika.
Kampuni hiyo iliambia mahakama kuwa KRC tayari imechukuwa ardhi yake kwa lazima lakini imenyimwa matunda ya fidia kwa vile pesa zake hazijatolewa kutokana na mizozo isiyoisha mahakamani.
“Kampuni inateseka na inaendelea kupata hasara kubwa kutokana na kuchukuliwa kwa lazima ardhi bila fidia inayohitajika,” ilisema.
Hata hivyo, Kahia Transporters na Trade Lead Ltd wanataka tathmini ya fidia iliyofanywa ifutiliwe mbali na NLC ifanye tathmini nyingine kabla fidia ilipwe.
Makampuni hayo mawili yamesisitiza kuwa pande zote lazima zisikizwe kabla ya mahakama kutoa maagizo ya malipo ya fidia .
Kulingana nao, kuna mzozo kwa vile pia wao wana hatimiliki na wameathiriwa na mradi wa SGR.
“Mlalamishi hana ardhi yoyote inayostahili kufidiwa. Kesi hii inafaa kutupiliwa mbali,” makampuni hayo mawili yalisema kupitia kwa mawakili wao.
Makampuni hayo yameshutumu NLC kwa madai ya kupotosha mahakama, na kuongeza kuwa baadhi ya hatimiliki ambazo sasa zimezua migogoro mahakamani kuhusu fidia zilitengenezwa kama njia moja ya kupata pesa za SGR kiharamu.
Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa NLC ilishughulikia mzozo huo kabla ya kutoa fidia hiyo na ilithibitisha uhalali wa hatimiliki ililokuwa likishikiliwa na Dopp Investment Ltd kupitia uamuzi wake wa Februari 25, 2016.
Stakabadhi zinaonyesha kuwa utafiti uliofanywa na NLC ulibaini kuwa jumla ya hekta 13.348 zilichukuliwa kwa lazima na serikali.
Zaidi ya hayo, rekodi za mahakama zinaonyesha kuwa kutokana na rekodi rasmi zilizopo, kipande kimoja cha ardhi kilifanyiwa utafiti na kusajiliwa mwaka 1991 huku kingine kikifanyiwa utafiti na kusajiliwa mwaka 2017.
Next article
MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa tambi (noodles)