Connect with us

General News

ODM yapuuza hatua ya Kingi kuitoroka akielekea kwa Ruto – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

ODM yapuuza hatua ya Kingi kuitoroka akielekea kwa Ruto – Taifa Leo

ODM yapuuza hatua ya Kingi kuitoroka akielekea kwa Ruto

CHAMA cha ODM kimepuuza hatua ya Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, kuhamisha chama chake cha Pamoja African Alliance (PAA) kutoka Muungano wa Azimio la Umoja One-Kenya.

Bw Kingi jana Jumanne alipokewa rasmi katika Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto, ambaye ni mgombeaji urais kwa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Gavana huyo ambaye anatumikia kipindi chake cha mwisho alitarajiwa kushirikiana na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho katika kampeni za urais za kinara wa ODM, Bw Raila Odinga eneo la Pwani.

Hatua yake ilijiri wakati ambapo Bw Odinga anatarajiwa kufanya ziara ya Pwani kuanzia leo.Mwenyekiti wa ODM tawi la Mombasa, Bw Mohammed Khamis, jana alisema hawakushtushwa na hatua ya Bw Kingi.

“Tulijua alikuwa amepanga kuondoka. Sisi tunaandaa mikutano ya hadhara ya chama eneo la Pwani ili tueneze ajenda yetu na kupigia debe kura ya urais katika Azimio la Umoja,” akasema Bw Khamis.

Ushawishi wa Bw Kingi katika Kaunti ya Kilifi unaaminika uliisaidia ODM kuzoa viti vyote vya kisiasa katika uchaguzi uliopita.

Akizungumza Jumanne, Dkt Ruto alisema sasa wanatarajia ushawishi huo wake utasaidia Kenya Kwanza kuzoa kura nyingi za urais pamoja na viti vingine katika uchaguzi wa Agosti 9.

Kufikia jana, Dkt Ruto alikuwa amevutia gavana mmoja pekee wa kaunti za Pwani upande wake.

Mbali na Gavana wa Kwale, Bw Salim Mvurya na sasa Bw Kingi, magavana wengine wanne waliobaki bado wanaegemea upande wa Azimio.

Aliyekuwa waziri msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, alitilia shaka athari ya kuondoka kwa Bw Kingi kwa umaarufu wa ODM katika eneo hilo.

“Bw Odinga bado ni maarufu kwa wakazi. Itikadi zake zimekwama akilini mwa wananchi,” akasema.

Uhusiano wa Bw Kingi na viongozi wa ODM ulianza kufifia alipoanzisha mipango ya kuunda chama chenye mizizi yake Pwani.

Wakati juhudi zake za kuunganisha vyama vidogo vya Pwani ili kuwe na chama kimoja kugonga mwamba, aliamua kuunda PAA, ambayo baadaye aliishirikisha katika Azimio na hivyo basi kumrudisha upande wa Bw Odinga ambaye alikuwa amekosana naye kisiasa.

Ukosefu wa uaminifu

Akizungumza Jumanne baada ya kukutana na Dkt Ruto, gavana huyo alisema uamuzi wa PAA kujiondoa Azimio ulisababishwa na kile alichotaja kuwa ukosefu wa uaminifu katika muungano huo unaoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga.

Mkataba wa Azimio uliweka masharti makali ambayo yangezuia vyama kujiondoa kabla ya uchaguzi ujao, lakini Bw Kingi alisema PAA haikuwa imeafikiana na mkataba huo ndiposa uwe rasmi.

Hii ni licha ya kuwa PAA iliorodheshwa rasmi katikaa gazeti la serikali kama chama tanzu cha Azimio.

“Matakwa ya kisheria ambayo yangetufanya kujiunga kikamilifu na Azimio hayangekamilika kwa sababu hatukupewa nakala ya makubaliano ili tuikabidhi kwa Baraza Kuu la chama chetu ipitishe inavyotakikana kwa katiba yetu,” akasema.

Kulingana naye, sababu zilizofanya wahame ni usiri mkubwa katika Azimio, vyama kulazimishwa kufuata maamuzi ya watu wachache, na ukosefu wa kujitolea kwa Azimio kutekeleza mahitaji ya Wapwani.

Bw Kingi alidai kuwa uamuzi wake kujiunga na Dkt Ruto ni kwa minajili ya kutekeleza masilahi ya Wapwani wala si kutaka kugawiwa mamlaka.

Hata hivyo, imebainika mikataba ya Kenya Kwanza imetoa mpangilio wa jinsi vyama vitagawana mamlaka ambapo UDA itapewa asilimia 30 ya vyeo serikalini, Amani National Congress (ANC) na Ford-Kenya kugawana asilimia 30, na vyama vingine vyote kugawana asilimia 40 zitakazobaki.