Orengo awashauri wanasiasa kuingia katika miungano kwa hiari na wadumishe utulivu
NA CHARLES WASONGA
SENETA wa Siaya James Orengo amewaonya wanasiasa na akawataka kukoma kujilazimisha katika kubuni miungano ya kisiasa kinyume na mapenzi yao.
Akiongea Jumanne, Aprili 26, 2022, katika bunge la seneti wakati wa kikao maalum kilichoitishwa kutoa fursa kwa maseneta kumuomboleza Hayati Mwai Kibaki, Bw Orengo aliwataka wanasiasa kuiga muungano wa kisiasa ambao mwendazake alibuni na kiongozi wa ODM Raila Odinga.
“Ndoa za kisiasa zinazolazimishwa huwa zinafeli. Nawaomba wanasiasa wa sasa kuiga mfano wa ndoa ya kisiasa kati ya Kibaki na Raila iliyoundwa kutokana na makubaliano ya hiari kati yao,” Bw Orengo alisema, huku akionekana kurejelea miungano ya sasa ya kisiasa ya Azimio la Umoja-One Kenya na Kenya Kwanza.
Wakati wa kikao hicho, seneta huyo wa Siaya na mwenzake wa Bungoma Moses Wetang’ula walitoa kumbukumbu ya kamati ya upatanishi uliochangia kuundwa kwa serikali ya Muungano wa Kitaifa baada ya uchaguzi wa 2007.
Serikali hiyo iliundwa ghasia zilipotokea baada ya Bw Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais ambapo Kibaki alitangazwa kuwa mshindi.
Maseneta Orengo, Wetang’ula na Sam Ongeri walikuwa wanachama kamati hiyo ya upatanishi iliyoongozwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) marehemu Kofi Annan.
Kando na Profesa Ongeri, wengine waliokuwa wanachama wa kamati hiyo wakiwakilisha mrengo wa Kibaki, walikuwa kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na aliyekuwa Seneta wa Makueni marehemu Mutula Kilonzo.
Kando na Bw Orengo, wale ambao waliwakilisha upande wa Bw Odinga katika kamati hiyo walikuwa ni; aliyekuwa mkuu wa Utumishi wa Umma Sally Kosgei, Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.
Katika mchango wake, Bw Wetang’ula alisema japo makubaliano yalifikiwa baada ya mvutano wa muda mrefu, Bi Karua alikataa kutia saini stakabadhi ya mwisho.
“Karua ndiye alikuwa mwanachama mwenye msimamo mkali kiasi kwamba hata baada ya mapatano kufikiwa, hakukubali. Hii ndio maana alikataa kuhudhuria sherehe ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo katika ukumbi wa KICC, Nairobi,” akaeleza.
Maseneta walimmiminia sifa Kibaki wakimtaja kama Rais ambaye aliweka msingi wa maendeleo ya kiuchumi ambayo taifa hili imefikia tangu Rais Uhuru Kenyatta alipochukua usukani.
Awali, Spika wa Seneti Kenneth Lusaka alimsifu Hayati Kibaki akimtaja kama ambaye aliongoza taifa hili wakati ambapo taifa hilo lilikumbwa na misukosuko mikubwa ya kisiasa na kiuchumi.
Aidha, akasema, ni wakati wa utawala wa Kibaki ambapo Kenya alipata Katiba ya sasa ambayo ilizinduliwa rasmi mnamo Agosti 27, 2010.
“Kenya na ulimwengu kwa ujumla imepoteza kiongozi shupavu, mwanauchumi mahiri na mwanasiasa ambaye aliweka masilahi ya wananchi mbele ya masilahi yake binafsi,” Bw Lusaka akaeleza.