Connect with us

General News

Pigo kwa Sossion akizama mchujoni – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Pigo kwa Sossion akizama mchujoni – Taifa Leo

Pigo kwa Sossion akizama mchujoni

NA VITALIS KIMUTAI

KATIBU mkuu wa zamani wa Chama cha Kitaifa cha Walimu nchini (KNUT) Bw Wilson Sossion amepokea pigo kuu kisiasa, katika miezi 10 iliyopita, akipoteza vita viwili vikuu ambavyo vina uhusiano na utumishi wake wa umma.

Ijumaa iliyopita, Bw Sossion hakuweza kustahimili machungu ya kushindwa katika mchujo wa chama cha UDA wa kutafuta mpeperusha bendera ya kuwania Useneta mjini Bomet.

Mwanasiasa huyo aliishia kurusha cheche kali za matusi, kuhusiana na madai ya udanganyifu katika zoezi hilo.

Alikuwa na machungu ya kushindwa na wakili na mwanafunzi wake wa zamani Bw Hillary Sigei, ambaye alimshinda kwa kura 32,129 na kuwa mpeperusha bendera wa Useneta kaunti hiyo.

Bw Sigei alikuwa na kura 77,500, akafuatwa na Dkt Christopher Lang’at na kisha Bw Sossion akavuta mkia kwa 45,371.

Haya yamejiri baada ya karibu mwaka mmoja tangu ajiondoe kwenye uongozi wa KNUT, baada ya kupoteza ufuasi mkubwa kutoka kwa maafisa wa matawi yote kutoka humu nchini.

Mwishoni mwa uongozi wake wanachama walikuwa wamepungua kutoka 187,000 hadi 15,000. Isitoshe ada ya uananchama ilikuwa imepungua kutoka Sh147 milioni kila mwezi hadi Sh12 milioni.

“Chama cha UDA kimejaa watu fisadi na wezi ambao wananuia kuweka wanabiashara wenzao uongozini. Nia yao ni wawasaidie kuiba raslimali za umma baada ya uchaguzi,” alilalamika Bw Sossion.

Bw Sossion ambaye alikuwa amejawa na hasira katika ukumbi wa St Bakhita mjini Bomet uliokuwa kituo cha kuhesabia kura, alisema kuwa Baraza la Taifa la Uchaguzi (NEB) lilikuwa limeanza safari ya kuangusha meli ya UDA hata kabla ya Uchaguzi wa Agosti 9 kuwadia.

“Hatutakubali matokeo na tutawaagiza wafuasi wetu wampigie mmoja wetu kura kama mgombeaji huru, kwenye uchaguzi mkuu,” alisema Bw Sossion aliyekuwa na Seneta Christopher Langat ambaye pia alipinga matokeo ya mchujo huo.

Bw Sigei alikuwa mwanafunzi katika shule ya upili ya wavulana ya Tenwek ambako Bw Sossion alikuwa mwalimu.

Bw Sigei baadaye alikuwa wakili wa Bw Sossion, na anamwakilisha hadi sasa katika kesi zinazoendelea kortini.

Alipopokelewa na Naibu wa Rais William Ruto jijini Nairobi mwaka 2021, wengi walishtuka kwani alikuwa mmoja wa waliokuwa wakipigia debe mchakato wa kubadilisha katiba (BBI) kusini mwa bonde la ufa, ambao Dkt Ruto alikuwa anaupinga.

Licha ya kumtema Bw Raila Odinga na kuandamana na Dkt Ruto kupigia upatu muungano wa Kenya Kwanza, amepata pigo kisiasa katika mchujo wa UDA, ambao umedaiwa kuwa na udanganyifu mwingi.

Bw Sossion alipoteza katika mchujo huo kwa kushindwa kuwashawishi walimu kumuunga mkono na kuendelea kupigana na uongozi wa KNUT kwenye matawi na kitaifa licha ya kustaafu.