POLISI mjini Thika mnamo Jumanne, walinasa bangi kwenye magunia saba yaliyokuwa yamefichwa ndani ya gari.
Kulingana na polisi wa kituo cha Kimuchu, Makongeni, Thika, kaunti ya Kiambu, wananchi walishuku gari moja lenye nambari KCH 657E lililosimama kando ya barabara.
Kamanda wa polisi kaunti ya Kiambu Bw Perminus Muchangi Kioi alithibitisha tukio hilo akisema bangi hiyo ilikuwa ya thamani ya Sh2.5 milioni.
Afisa huyo alieleza ya kwamba washukiwa wenye gari hilo walitoroka baada ya kugundua kuwa walikuwa wakisakwa na polisi.
Amesema kuwa tayari gari hilo limezuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Kimuchu huku wakiwasaka washukiwa hao.
Bangi kwenye magunia saba yakiwa yamefichwa ndani ya gari. PICHA | LAWRENCE ONGARO
Afisa huyo ametoa onyo kali kwa walanguzi wa dawa za kulevya akisema siku zao zimewadia.
“Tayari tunaendelea na uchunguzi ili kuwanasa washukiwa waliohusika na kupatikana na bangi hiyo. Tutahakikisha wametiwa nguvuni,” alifafanua kamanda huyo wa polisi.
Aliwapongeza wakazi wa Kimuchu kwa ushirikiano mzuri walioonyesha huku akiwataka wawe na msimamo huo huo.
Tayari polisi wa upelelezi ( DCI), wanaendelea kufanya uchunguzi kubainisha mahali bangi hiyo ilikotolewa.
Gari hilo lilibururwa hadi kituo cha polisi cha Makongeni mjini Thika, huku bangi hiyo ikiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Kamanda huyo alisema washukiwa hao wakinaswa watahojiwa kabla ya kupelekwa mahakamani kujibu mashtaka.
“Ninapongeza juhudi zilizochukuliwa na wananchi kwa kupiga ripoti baada ya kushuku gari lililosimama kando ya barabara,” alisema kamanda huyo wa polisi.
Alisema serikali haitapumzika hadi iwanase washukiwa hao. Kwa hivyo aliwarai wananchi washirikiane nao ili kuona ya kwamba inafanikiwa katika harakati zake.