TAHARIRI: Pombe haramu ni janga kwa taifa letu
NA MHARIRI
KILA mwaka visa vya watu kufa au kuathiriwa na pombe haramu huwa vinaripotiwa.
Katika kisa cha hivi punde, watu sita walifariki dunia baada ya kunywa pombe iliyowekwa sumu kaunti ya Bungoma.
Wengine kadhaa wamelazwa katika hospitali hiyo wakiwa hoi baada ya kuathiriwa na pombe hiyo.
Mwaka 2021, watu kadhaa walikufa baada ya kunywa pombe haramu kaunti ya Nakuru.
Katika kisa hicho, maafisa kadhaa wa utawala na usalama walichukuliwa hatua za nidhamu kwa utepetevu kazini.
Licha ya serikali kuwachukulia hatua, ili wawe funzo kwa maafisa wa maeneo mengine wanaoruhusu upikaji na uuzaji wa pombe haramu, inaonekana hawakupata funzo.
Hii ni kwa sababu visa hivi vinaendelea kuongezeka nchini ishara kwamba maafisa wanaopaswa kuchukua hatua kuangamiza biashara hii wametelekeza kazi yao au wanahongwa na wanaoifanya.
Pombe haramu, sawa na dawa za kulevya, imeathiri vijana wengi, wanaume na wanawake na kuwafanya wasichangie katika ujenzi wa taifa.
Uraibu huu ni pacha wa ukosefu wa usalama. Unachangiwa na kupaliliwa na umasikini ambao serikali inafaa kujukumika kuukabili. Labda umefika wakati wa kutangaza pombe haramu kuwa janga la kitaifa.
Kufariki kwa watu kila mwaka, gharama ya kutibu waathiriwa na hasara ambayo nchi inapata kutoka na vileo haramu sio jambo la kawaida.
Ni janga la kujitakia kwa vile kama nchi, tumeshindwa kuimarisha uchumi na kutumbukiza asilimia kubwa ya raia katika umasikini kiasi za kuzama katika ulevi wa kupindukia.
Hatutaki kuwa manabii wa maangamizi, lakini tunayoshuhudia yanaweza kuwa mwanzo wa hali mbaya zaidi ikiwa uchumi utaendelea kudorora. Kama nchi, tunahitaji mageuzi makubwa katika vita dhidi ya vileo haramu.
Next article
Zogo ODM ikimpa Boga tiketi mboga Kwale