Connect with us

General News

Presenta Ali na shughuli zake za Vlogging Kanairo – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Presenta Ali na shughuli zake za Vlogging Kanairo – Taifa Leo

KIPWANI: Presenta Ali na shughuli zake za Vlogging Kanairo

NA SINDA MATIKO

MWITE utakavyo, Presenter Ali, au Entertainment P.A ila wazazi wake wanamfahamu kama Muslim Ali.

Kazaliwa na kulelewa Bombolulu, Mombasa ila kwa sasa yupo Nairobi, almaarufu ‘Kanairo’ anakohangaika na shughuli za Vlogging. Kipwani tuligonga naye kitaa na kuishia kumaliza siku naye hivi:

Asalaam Aleikum, bro, mwezi mtukufu wa Ramadhan wakupeleka vipi?

Waaleikum Msalaam Warahmatullah Wabarakatuhu. Nashukuru Alhamudhulilah Mwenyezi Mungu anasaidia. Mwezi huu ni muhimu sana katika maisha yangu. Ni mwezi ambao unanipa fursa ya kujiweka karibu zaidi na Allah, jamaa zangu pamoja na marafiki.

Baadhi ya mambo ambayo unaepukana nayo kwenye Ramadhan ni kama yapi?

Huwa najitahidi sana kuepukana na vishawishi potofu na pia maskendo skendo hivi, wajua tena sisi tupo kwenye shughuli hizi za kuvlogu na mambo kama hayo. Lakini pia kuna vitabia vya kwangu ambavyo huwa najipiga msasa na kujaribu kuondokana navyo. Kama sasa najitahidi sana kupunguza uraibu wangu wa kutumia muda mwingi nikicheza cheza na simu.

Mara ya kwanza tunakutana ilikuwa ni kwenye uzinduzi wa Guiness Smooth, ulikuwa mtangazaji wa TV. Ndio ulikuwa unaanza shughuli hizi za kuwa mtangazaji au?

Enhee! Nakumbuka na kama sikosei ilikuwa 2019. Hapo nilikuwa tayari nimeanza mishemishe hizi. Kazi yangu ya kwanza ya utangazaji niliipata 2017 nilipofanya kazi kwenye kituo cha Y254 kama ulipata kuisikia. Kipindi tunakutana, nilikuwa tayari nimeajiriwa na Switch TV na kufanya kazi kwa miaka miwili.

Uanahabari umesomea chuoni au ilitokea tu?

Ilitokea tu, nimetamani shughuli hizi tangu utotoni. Nilipenda sana kuwa mtangazaji wa redio ila nikaishia kwenye runinga. Nakumbuka nilikutana na mwanahabari akiwa kabeba camera na tripod nikamwelezea matamanio yangu ya kuwa mwanahabari. Miezi michache baadaye nikafanikiwa kupata fursa kama intern kwenye kituo cha televisheni alichokuwa akifanya kazi jamaa na ukawa ndio mwanzo wa safari yangu ya uanahabari.

Kwa sasa wewe ni Vlogger, uliishiaje huku?

Sijaanza leo mishemishe ya kuwa vloga. Toka nikiwa nafanya kazi Y254, nilikuwa navlogu kwa kusitasita. Niliamua kuzamia huko kabisa miezi kadhaa kabla ya kituo cha Switch TV kufungwa. Nilijiuzulu kazi yangu kama presenta. Nafikiri ni moja kati ya maamuzi bora niliyowahi kufanya katika maisha yangu.

Sasa hivi kila mtu anaparamia kuwa Vloga, wakati ni tasnia iliyoishi kuwa ya wachache kwa miaka mingi sana. Hivi unafikiri ni kwa nini?

Ni kwa sababu wanaona mavloga wakiendesha maisha yao vizuri tu kupitia chaneli zao kwenye YouTube. Vijana wengi wajua hawana kazi kwa hiyo kila mtu anajitahidi kujipatia riziki.

Wewe ongezeko la mavloga kila uchao halikupi hofu ya ushindani?

Wala kabisa. Mwanzo ningetamani kuwaona vijana wengi zaidi wakigeukia shughuli zetu hizi. Kuna mambo mengi ya kuangaziwa ambayo watu wanataka kuona na kusikiza. Sio lazima uangazie masuala ya burudani kama mimi, unaweza ukazamia kwenye masuala ya upishi, afya na mazoezi, biashara, utandawazi nakadhalika.

Mbona kama nahisi ongezeko hili la mavloga ni kwa sababu wapo watu wanataka kutengeneza pesa za haraka?

Ni kama nilivyotanguliza. Vijana wengi hawana kazi lakini pia wametuona baadhi yetu tukijichumia riziki na maisha yakaenda. Inawezekana wapo wenye tamaa ya kutengeneza pesa haraka ila kama ndio lengo basi hawatadumu sana. Kuwa vloga lazima upende kazi yenyewe. Ni kama kipaji vile hivyo lazima uwe na msukumo sahihi ndio utafanikiwa.

Itakuwa mishemishe ya kuwa vloga inalipa vizuri sana, ila najua pia lazima mtu awe na timu, je mpunga huo unatosha?

Huwezi kuwa vloga ukafanya kila kitu mwenyewe utahitaji timu. Kipato kipo, shughuli inalipa vizuri tu ila utahitaji kuweka juhudi kubwa na iwe ni juhudi ya mfululizo. Ukifanya hivyo utajihakikisha fedha za kutosha zako wewe na pia mgao wa kikosi chako. Mbali na fedha, uwepo wa timu humsukuma mtu sana kuboresha kazi sababu wazo linakuwa sio la ubongo mmoja bali bongo kadhaa. Kuna siku utajihisi hutaki kufanya lolote, timu inakusukuma.

Leo ukipata ajira nyingine runingani, harakati za vloga vipi, utaacha?

Duh! Hili nalo nzito. Najua kazi zingine hubana ila kama itaniruhusu niendelee na shughuli zangu za kuwa Vloga nitaikubali ofa. Sababu mwisho wa siku la msingi ni kuwa na uwezo wa kujiajiri badala ya kuajiriwa.

Mavloga wa burudani wengi wanaonekana kupenda kusukuma akaunti zao kwa taarifa za kiki, hili linakuathiri vipi?

Pana haja ya kuwepo na udhibiti wa misingi ambayo vloga wanapaswa kuzingatia kwenye utendaji wao. Hao unaowazungumzia ni mavloga ibukia. Hawana uhalisia wa kazi zao, wanajaribu kuwaiga wengine. Hawana zile nidhamu za taaluma. Wachache hawa wanatufanya mavloga wengine tuonekane watu ovyo tusiojielewa.

Mpaka sasa safari hii imekufunza nini?

Kwamba soko la mitandaoni hubadilika badilika kila kukicha, lazima uwe makini sana kuwasoma watu wanataka nini, ukawaletea habari hizo. Lakini pia ni lazima uwe mwepesi kwenye kuandaa kazi zako sababu soko lina ushindani mkubwa. Unatakiwa kuwa rada muda wote, kuhakikisha ni wewe unayeibuka na taarifa za nguvu kabla ya wenzio.

“Mimi ni P.A (presenter Ali), ila kumbuka A is always for the Amazing” , wajua kujichocha sana mzee baba. Hicho kibwagizo wakati unaaga huwa chanifurahisha

Hahaha nashukuru bro. Kwenye kazi hizi ubunifu ni kitu muhimu sana. Nafurahia kusikia hivyo, inaonyesha nakwenda vizuri. Mbali na hayo huwa nasema vile kama vile kuhamasisha umma. Tunaishi nyakati ambayo kuna chuki nyingi sana. Watu hawatakiani mema, wivu umetawala na hali hii inatisha kwa kweli.

Mmh! pamoja na yote hayo, niambie kitu. Hivi Presenter Ali ni nani haswa, umekulia wapi?

Majina kamili ni Muslim Ali. Nimezaliwa mtaa wa Bombolulu, Mombasa nikalelewa kidogo Makindu, kisha Makueni halafu nikajikuta Nairobi. Shule ya msingi nimesomea Kiambani na kidato nikasomea Ofafa Jericho Nairobi kwa hiyo maisha ya mtaa Nairobi, Mombasa naelewa sana. Nimerudi darasani tena nipo chuoni nasomea shahada ya Urban Planning.

Mwaka huu umenizengua, wajua kwa miaka mingi ulificha mahusiano yako, kisha boom! Ukaamua kumposti shemeji yetu. Mmh! Aki mapenzi wewe?

Haha! Hamna bro, sikuwahi kumficha mtoto wa watu mimi.

Miaka yote hiyo sijamposti dada wa watu nimekuwa singo. Niamini nikikuambia sikuwa na mwenza muda wote huo hadi nimepata huyo shemeji yako.

Kwa hiyo shemeji umejuana naye juzi tu, mapenzi yakakulemea ukaamua kumpostia umma?

Haha! Naona umeamua kunizengua sasa. Hamna, mrembo tumefahamiana naye kwa miaka minne sasa, ila hatukuwa kihivyo tulivyo sasa, kwa hiyo nyuma kidogo nisingeliweza kumposti. Namposti sasa baada ya kupiga hatua kwenye mahusiano yetu.

Kwa kufahamu presha na chambo za mitandaoni, huogopi athari zake kwenye uhusiano wako?

Wala sina hofu. Zaidi ya picha picha hizo za kilavi davi ninazoposti, hamna anayefahamu yanayoendelea nyuma ya pazia. Mahusiano yetu ni siri kubwa sana. Itakuwa shughuli kubwa kwa yeyote atakayejaribu kuchunguza mahusiano yetu sababu hatafanikiwa kupata udaku wa aina yeyote.

Kwa namna unavyopiga pamba, mwonekano na umaarufu huna kabisa huruma kwa wengi uliowavunja mioyo. Wanasemaje huko kwenye DM yako hao masinyorita uliowaumiza mtima?

Haha! Duh! Leo naona umeamua kunichachishia kaka. Ndio maisha wajua. Sasa ningefanyeje. Huwezi kumfurahisha kila mtu haiwezekani. Ila pamoja na hilo, nawaheshimu sana mashabiki zangu wa kike. Kwenye DM huwa najitahidi sana kuwajenga mazingira ya uelewa huo na kwamba haya ni maisha, kila mtu kaandikiwa wake.

Nivyocheki posti zako Instagram, naona penzi lenu linakwenda kwa kasi ya 5G, hadi lanitia wivu, sasa naomba kujua kitu Sheikh, Nikah ndio tuisubirie lini sasa?

Hahah, InshaaAllah harusi ni tukio la kheri ndoa nayo ni majaaliwa. Inaweza ikatoke wakati wowote kwa mapenzi ya Allah. Tusubiri na tuishie kuombeana dua kakangu.

Kila la kheri Sheikh ila usisahau kunialika siku ya siku, kanzu nitaazima.

Haha! Inshallah Amin! Tumwombe Allah atujalie kheri tushereheke siku hiyo.