Presha kwa Ruto na Raila kuhusu wagombea wenza
ONYANGO K’ONYANGO na LEONARD ONYANGO
WAWANIAJI wa urais wamejipata katika njiapanda baada ya kutekwa nyara na baadhi ya jamii zinazotaka kupewa nafasi ya mwaniaji mwenza.
Naibu Rais William Ruto na mwaniaji urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Bw Raila Odinga, wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kuteua wawaniaji wenza wao bila kuzua mgawanyiko.
Viongozi wa Mlima Kenya wamekuwa wakishinikiza wawili hao kuteua mwaniaji mwenza kutoka eneo hilo.
Maeneo ya Magharibi na Ukambani pia yanang’ang’ania nafasi hiyo.
Dkt Ruto na Bw Odinga wana hadi Mei 16 kutangaza wawaniaji wenza wao.
Kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula hivi majuzi walifichua kuwa eneo la Magharibi litapata asilimia 30 ya serikali iwapo muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto utashinda Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.
Ufichuzi huo unadhihirisha jinsi Dkt Ruto alivyoshikwa mateka na viongozi wawili hao.
Bw Mudavadi alipokuwa katika Kaunti ya Vihiga wiki iliyopita alisema kuwa eneo la Magharibi litatengewa asilimia 30 ya nyadhifa serikalini, Idara ya Mahakama na Bungeni.
Alisema kuwa mawaziri sita kati ya 22 na asilimia 30 ya mabalozi na maafisa wa Idara ya Mahakama watakuwa watu kutoka eneo la Magharibi.
Kwa upande mwingine, viongozi wa Mlima Kenya wakiongozwa na mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua, wameshikilia kuwa sharti mmoja wao awe mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto.
Bw Gachagua amewahi kunukuliwa akisema kuwa mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto alijulikana kabla ya Bw Mudavadi kuamua kumuunga mkono mapema mwaka huu.
Katika mrengo wa Azimio, kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ametishia kuwa Bw Odinga atapoteza iwapo hatamteua kuwa mwaniaji mwenza wake.
Katibu wa Baraza Kuu la Azimio Junet Mohammed jana Jumatano alitangaza majina ya watu saba watakaoshauri Bw Odinga kuhusu mtu anayestahili kuwa mwaniaji mwenza wake.
Kamati hiyo inajumuisha makasisi wastaafu Askofu Peter Njenga, Askofu Zacchaeus Okoth, Seneta wa Kitui Enoch Wambua, Katibu Mkuu wa Narc Kenya Michael Orwa, mwanasiasa mkongwe Noah Wekesa, Sheikh Mohamed Khalifa na Bi Beatrice Moen.
Mkurugenzi Mkuu wa Sekretariati ya Kampeni za Bw Odinga, Elizabeth Meyo atakuwa katibu wa kamati hiyo ambayo imetakiwa kupendekeza majina ya watu wanaostahili kuwa wawaniaji wenza kufikia Mei 10, 2022.
“Watu wanajua vyema kwamba Raila akiteua Kalonzo kuwa mwaniaji mwenza wake atapata ushindi wa kishindo lakini akiacha Kalonzo kutakuwa na shida,” Bw Musyoka alinukuliwa akisema aliokuwa mjini Kitui, Jumapili.
Bw Wambua Jumatatu alisema kuwa Bw Odinga atapoteza zaidi ya kura milioni 1.8 za Ukambani iwapo hatateua Bw Musyoka kuwa mwaniaji mwenza wake.
Wengine wanaotegea nafasi ya mwaniaji mwenza wa Bw Odinga ni mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth, kinara wa Narc Kenya Martha Karua, Waziri wa Kilimo Peter Munya na Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi.
Wanaomezea mate nafasi ya mwaniaji mwenza wa Dkt Ruto ni Bw Gachagua na wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Alice Wahome (Kandara), Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru, Seneta Kindiki Kithure (Tharaka Nithi) na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.