Connect with us

General News

Raila aitwa kuhojiwa NCIC kwa kusema hataki ‘madoadoa’ Wajir – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Raila aitwa kuhojiwa NCIC kwa kusema hataki ‘madoadoa’ Wajir – Taifa Leo

Raila aitwa kuhojiwa NCIC kwa kusema hataki ‘madoadoa’ Wajir

NA WANGU KANURI

TUME ya Uwiano na Utangamano (NCIC) imemwelekeza kinara wa ODM Raila Odinga ajifikishe baada ya kutumia neno ‘madoadoa’ alipokuwa akifanya kampeni zake.

Raila alitumia neno hilo Jumatano alipokuwa katika kaunti ya Wajir.

“Tunataka wote hapa Wajir wachaguliwe kwa Azimio. Tunataka hapa Wajir iwe eneo la Azimio. Mpo tayari? Hatutaki madoadoa hapa Wajir,” akasema akiwarai wakazi wa kaunti hiyo. Kulingana na mwenyekiti wa NCIC, Dkt Samuel Kobia, neno ‘madoadoa’ huchukuliwa kuwa neno la chuki nchini Kenya.

Amri ya NCIC inakuja siku moja baada ya baadhi ya viongozi akiwemo seneta wa Tharaka-Nithi Kithure Kindiki kuambia Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) imtie mbaroni Raila kufuatia matumizi ya neno madoadoa.

“Tunasema hakuna sheria moja ya watu wa Azimio na nyingine ya watu wa Kenya Kwanza. Tunaomba vikosi vya serikali, vile walisukumu Linturi wakati alitumia jina madoadoa alipokuwa Eldoret, waharakishe washike kiongozi wa Azimio. Hata yeye alale ndani,” akasema seneta huyo wa Tharaka Nithi.

Mapema mwaka huu, seneta wa Meru, Mithika Linturi akiwa kwenye mkutano wa kisiasa wa William Ruto alisema ‘madoadoa’ yaondolewe katika bonde la ufa.

Matamshi yale yaliwafanya Wakenya pamoja na viongozi kumshutumu huku Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji akiamuru uchunguzi uliomfanya akamatwe.

Hata hivyo baada ya uchunguzi kukamilika na kufikishwa kortini mara kadhaa, Bw Linturi aliachiliwa kwa dhamana ya Sh5 milioni au dhamana ya pesa taslimu ya Sh2 milioni.