Connect with us

General News

Raila atajali Mlima Kenya, wasema washirika wake – Taifa Leo

Published

on

[ad_1]

Raila atajali Mlima Kenya, wasema washirika wake – Taifa Leo

Raila atajali Mlima Kenya, wasema washirika wake

NA CHARLES WANYORO

VIONGOZI watatu kutoka Mlima Kenya wamewarai wenyeji kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kuwania urais mwaka ujao ili kulihakikishia eneo hilo ustawi wa kiuchumi.

Watatu hao—mwanasiasa Peter Kenneth, mbunge Maoka Maore (Igembe) na Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru, Bw Joseph Kaberia—walisema wana imani kwamba Bw Odinga hatalitenga eneo hilo baada ya Rais Kenyatta kuondoka uongozini.

Wakizungumza katika Shule ya Msingi ya Murungene, Kaunti ya Meru, wakati wa fainali za kandanda za Kombe la Chapa Dimba na RMM, walisema wametathmini ahadi ambazo zimetolewa na Bw Odinga kuhusu eneo hilo, ambapo wanaamini ndizo bora ikilinganishwa na wengine.

Bw Kenneth alisema umaarufu wa Bw Odinga katika eneo hilo umeimarika kutokana na ahadi ambazo amekuwa akitoa kwa wenyeji kwenye ziara ambazo amekuwa akifanya kuupigia dene mpango wa Azimio la Umoja.

Walisema wana furaha kwamba kupitia muungano huo, watashirikishwa na kupewa nafasi sawa na washirika wengine. Walisema wanaamini vile vile watakuwa wakijumuishwa kwenye maamuzi muhimu kuhusu maslahi ya eneo hilo.

“Wenyeji kutoka Mlima Kenya watakuwa na jukumu muhimu sana la kupigania maslahi yao. Bw Odinga anajali maslahi ya nchi yote kwa jumla, wala si maslahi yetu pekee. Huo ndio uongozi ambao taifa hili linahitaji. Tumefanya mikutano mingi nchini kuupigia debe mpango wa Azimio la Umoja, ambapo tunafahamu kuwa wengi wanatuunga mkono. Wanataka kuwa mahali ambapo watahisi wakiwa salama,” akasema Bw Kenneth.

Viongozi walimlaumu Naibu Rais William Ruto kwa kuwa na machungu dhidi ya watu wanaopinga nia yake ya kuwania urais. Walionya huenda Dkt Ruto akalitenga eneo hilo ikiwa ataibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.

“Tunawaomba kuwapiga darubini vigogo wote ambao wametangaza watawania urais. Hebu tuangalie ni kiongozi yupi ambaye tutakuwa salama chini yake. Bw Odinga anakuja kwetu akiwa mnyenyekevu kinyume na wengine wanaokuja huku wakizungumza kwa ukali na uchungu mwingi. Je, ni yapi yatatufika akichukua uongozi? Tutateseka,” akaonya Bw Kenneth.

Bw Maore alisema wanamkwepa Dkt Ruto kwa sababu kwa mara kadhaa, amewatukana washindani wake. Walisema hiyo ni ishara ya kukwepa kuulizwa maswali muhimu kuhusu uwajibikaji wake.

“Ukimwona kiongozi akiwatukana washindani wake, hawataki kuulizwa maswali muhimu kuhusu vitendo vyao hapo awali. Hawatoi picha halisi kuhusu jinsi watakavyotimiza ahadi zao baada ya kuchaguliwa,” akasema Bw Maore.

Bw Kenneth alisema eneo hilo linahisi litakuwa salama chini ya Bw Odinga kutokana na utendakazi wake.

“Baadhi yetu hatumuungi mkono Bw Odinga kimakosa. Tupo hapo kwa sababu tunaamini ndiye kiongozi anayefaa,” akasema.

Mwanasiasa huyo ni miongoni mwa viongozi wanaopigiwa debe kuwa mgombea-mwenza wa Bw Odinga.